Msigwa aridhishwa ujenzi ofisi ya wizara yake

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi za Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo linalojengwa katika eneo la Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.

Amesema kasi hiyo inatoa matumaini kwa jengo hilo kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni 2024 kama ambavyo Serikali imeelekeza.

Msigwa amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua mradi huo wa ujenzi leo Februari 7, 2024 huku akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi na Watumishi wa Wizara hiyo.

“Ujenzi umefikia takribani asilimia 82 na kasi inaridhisha, tutafanya ukaguzi kila wiki na hatutaki kutoa muda wa nyongeza kwa mkandarasi nje ya muda uliopangwa. Leo nina furaha kwa hatua za mradi ulipofikia”. amesema Katibu Mkuu Msigwa.

Aidha,Katibu Mkuu Gerson Msigwa ametoa pongezi kwa mkandarasi wa mradi huo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) akionesha kuridhishwa na ubora wa kazi ya ujenzi wa mradi huo akibainisha kuwa mbali na jengo la ofisi za wizara la ghorofa nne kutakuwa na viwanja vidogo vya mpira wa kikapu, mpira wa miguu, netiboli na vitu mbalimbali katika eneo la mbele ya jengo hilo vinavyowakilisha Sekta zinazosimamiwa na wizara hiyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button