Msigwa: Miradi Dodoma haijasimama
MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Dodoma inaendelea vizuri.
Msigwa pia amewahakikishia Watanzania pamoja na wadau wa maendeleo kuwa mpango wa serikali kuhamia Dodoma hakuna kilichosimama na unaendelea vizuri.
Msigwa ameyasema hayo leo Januari 15 jijini Dodoma, akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muendelezo wake wa Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali na kusema kuwa jumla ya Sh bil.331 zimetolewa na serikali kwa miradi mbalimbali mkoani Dodoma.
“Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya Sh bil.331 zimetengwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Dodoma na mpaka sasa Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan ameshatoa jumla ya Bil.43/- kwa miradi mbalimbali ambayo imeshafikia asilimia 83,” amesema Msigwa.
Amebainisha kuwa baadhi ya miradi inayoendeleza kutekelezwa ni pamoja na miradi ya elimu, ambapo serikali imetoa jumla ya Sh bil.6.8 kujenga madarasa 339, ujenzi wa barabara ya mzunguko ambayo imefikia asilimia 20 mpaka sasa.
Miradi mingine ni Chuo Cha Ufundi Dodoma, kinachotarajiwa kuchukua wanafunzi 500, ambacho mpaka sasa kimefikia asilimia 75.
Miradi ya kilimo ya umwagiliaji pia ni miongoni mwa miradi iliyotengewa fedha ambapo Wilaya ya Mpwapwa inamradi wa umwagiliaji wenye gharama ya jumla ya Sh Bil.
27 na Wilaya ya Chamwino kuna mradi wa Sh Bil.11, ambapo itakapokamilika utasaidia kuongeza uhakika wa chakula.