“Msikae kimya,dereva akivunja sheria tuambieni”

MANYARA: Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani wilayani Mbulu mkoani Manyara limewataka abiria wa mabasi kutosita kutoa taarifa za madereva wanaokinzana na sheria za usalama barabarani kwani ni haki na wajibu wao kisheria na watazifanyia kazi ili kuzuia ajali za barabarani

Hayo yamesemwa leo Desemba 28,2023 na  Mtendaji wa polisi kikosi hicho, dawati la elimu usalama Koplo (CPL), Ester Mwijarubi wakati akitoa elimu ya haki na wajibu wa abiria kwa madereva, abiria na kondakta wa mabasi katika stendi kuu Manyara.

Pia amewataka abiria kufahamu kuwa ni haki na wajibu wao kutoa taarifa za madereva wanaoendesha vyombo vya moto bila kuzingatia sheria hususani  michoro na alama za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuleta madhara kwao na vyombo hivyo

“msikae kimya, mkaogopa, dereva akivunja sheria tuambieeni ili tuchukue hatua ndio kazi yetu ” amesema Mwijarubi

Aidha, ametoa onyo kali kwa madereva na kondakta wanaotumia lugha zisizofaa kwa abiria ikiwemo lugha za matusi na kuwaomba abiria kutowafumbia macho madereva wa namna hiyo.

Jeshi la polisi kikosi cha usalama barabarani kupitia watendaji wake wa dawati la elimu usalama wilayani humo wamekuwa bega kwa bega katika kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji  mbalimbali wa barabara ikiwemo madereva wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu na abiria

 

Habari Zifananazo

Back to top button