Msimamo watolewa wizi wa vishikwambi

JESHI la Polisi limewataka walioiba vishikwambi wanavyotumia makarani wa sensa ya watu na makazi wavirudishe na limeonya mafundi simu waache kupokea vitu vya wizi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema kuna taarifa kwamba makarani hao wameibiwa vitendea kazi hasa vishikwambi katika mikoa ya Arusha na Katavi hivyo polisi linataka virudishwe mara moja na wengine wasithubutu.

Misime aliwaeleza waandishi wa habari kuwa polisi wanawatafuta wahusika ili wafikishwe mahakamani hivyo yeyote aliyehusika kuiba vifaa hivyo avirejeshe.

“Kuna baadhi ya watu huwa wanapokea mali za wizi hasa vifaa vya kielektroniki hususani wanaojiita mafundi ambao mara nyingi wanapokea vifaa kama hivyo. Sasa kama unataka kuendelea kuwa na uhuru wako wa kutokwenda magereza basi virejeshe kama umevipokea,” alisema.

Misime aliagiza makarani wa sensa wawe makini kwa kuwa uchunguzi wa polisi umeonesha kuwa baadhi yao wanaibiwa kwa sababu ya uzembe.

“Yale mafunzo waliyopewa, yale maelekezo ya kiusalama waliyopewa waendelee kuyazingatia ili wao wawe salama lakini pia vifaa vya serikali na kumbukumbu ambazo zimeshaingizwa katika vifaa hivyo ziweze kuwa salama,” alisema.

Misime alisema sensa inaendelea na hali ni shwari na kwamba polisi wataendelea kuimarisha doria na kama kuna mtu mwenye taarifa kuhusu watu wanaopanga kuiba vifaa kwa makarani wa sensa atoe taarifa kwa jeshi hilo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa aliagiza makarani wa sensa wavitunze vishikwambi na wakumbuke kuwa vifaa hivyo ni mali ya serikali na wana mikataba na serikali hivyo wahakikishe vinakuwa salama kwa ajili ya kazi wanayopaswa kuifanya.

“Kwenye kila kata kuna vishikwambi vya ziada ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanahesabiwa kwa kutumia teknolojia hii.

“Kazi inakwenda vizuri, mifumo yetu inafanya kazi vizuri, kwa wale ambao wako kwenye maeneo ambayo hayana mtandao wanakusanya taarifa wanasema off line wakifika sehemu yenye mtandao taarifa zinakuja makao makuu,” alisema.

Karani wa sensa katika Kata ya Majimoto, Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi, Kenan Kasekwa aliibiwa kishikwambi cha kumbukumbu za sensa usiku wa kuamkia Agosti 23 mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Catherine Mashala alisema karani huyo ambaye ni mwalimu alivamiwa, kitasa kikavunjwa na mtu akaingia chumbani kisha kubeba kifaa hicho, Sh 760,000, simu, redio na vitu vingine.

“Inavyoonekana alipuliza dawa ya kuwalaza usingizi yeye na familia yake. Yule mwizi aliingia chumbani akabeba mkoba, kishikwambi, fedha alizozikuta, simu na redio aina ya sabufa,” alisema Mashala.

Mratibu wa sensa katika Jiji la Arusha, Maneno Maziku alisema karani wa sensa, Sarapia Kiwango aliporwa kishikwambi eneo la Unga Limited usiku wa kuamkia Agosti 23 mwaka huu wakati anakwenda kuhesabu makundi maalumu.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button