MTWARA; Waumini wa dini ya Kikristo wametakiwa kuendelea kuishi maisha waliyoishi kipindi chote cha Kwaresma kwa kuwa na tabia ya kujitoa kwa ajili ya wengine, kuishi kwa upendo na mshikamano.
Akizungumza leo wakati wa ibada ya Pasaka, iliyofanyika Kanisa la Watakatifu wote Jimbo la Mtwara, Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara, Naibu Askofu wa kanisha hilo, Patrick Mwaya amewataka waumini hao, waendeleze waendeleze matendo mema hata baada ya kumalizika Kwaresima.
Amesema haitokuwa na maana kwa wao kurudi kwenye matendo maovu, wakati kipindi chote cha Kwaresma siku 40 waliishi kwa hofu ya Mungu na kujaliana.
Amewasisitiza kuishi kwa kujenga uhusiano mwema, mshikamano kuthaminiana na kujitoa kwa wahitaji kama Kristu alivyojitoa kwa ajili yao, lakini pia wadumishe moyo wa ukarimu na watu wote pale wanapoishi na wanaokutana nao maeneo mbalimbali.
‘’Sisi wote tumefunga tumejifunza tuwe na maisha ya ukarimu, upendo, kumcha Mungu, kwa hiyo tunakumbushwa na sikukuu kama hizi kwamba turekebishe mienendo yetu tuwe na mioyo yenye upendo kwa Mungu na kwa wenzetu,”amesema Mwaya.
Amewaomba waumini hao kuliombea taifa na viongozi wote kwa ujumla, ili maombi hayo yawaongoze viongozi kwenye kuleta maendeleo yaliyokusudiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala amewataka wananchi kuwatumia viongozi waliopo kwa kuwashauri, kushirikishana ili kuleta maendeleo kwenye mkoa huo.
Ameahidi kutoa ushirikiano,kuwatumikia wananchi bila kubagua, kutenda haki na kufanya kazi kwa utaratibu na maelekezo waliyopewa.