KATIBU Tawala wa Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, ametaka wanahabari na maafisa habari kwenye taasisi za serikali kuacha kufanya kazi kwa matukio pekee badala yake wajikite zaidi katika kuibua masuala mbalimbali yaliyopo kwenye jamii, hususani maeneo ya pembezoni.
Mwaluko alikuwa anafungua mkutano wa kuhamasisha wanahabari, kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa Program ya Shule Bora, inayotekelezwa katika mikoa tisa nchini kwa ufadhili wenye thamani ya Sh. Bilioni 271, unaotolewa na Serikali ya Uingereza.
“Natarajia kuona habari za kutosha kuhusu Program ya Shule Bora baada ya mkutano huu, msisubiri matukio nendeni vijijini mkaibue mambo yanayotakiwa kusikiwa na jamii,” amesema RAS.
Mratibu wa Program hiyo wa Mkoa wa Singida, Samwel Daniel, amesema utekelezaji wake unafanyika katika Shule zote 616 za awali na msingi mkoani humo, chini ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa muda wa miaka sita (Aprili 2022 – Machi 2027).

Kupitia program hiyo, Serikali inalenga kuongeza ubora wa elimu katika shule za awali na msingi, kwa kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na ujumuishi na kwa mujibu wa Daniel, mkutano kati ya Shule Bora na wanahabari wa Singida ni moja ya hatua za kufanikisha program hiyo.
Anasema wanahabari ni wadau ambao wanatarajiwa kushirikiana na wengine kufanikisha malengo, hivyo hawana budi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya Shule Bora ili wakahabarishe na kufundisha jamii kupitia vyombo vya habari.