“Msiweke nguvu elimu bora mkasahau maadili”

WAZAZI wengi wamekuwa wakielemewa na mzigo wa kuwalea watoto wao wakubwa na wajukuu ambao hawajapata ajira wala kujiajiri, ndio maana serikali imeamua kubadili mitaala itakayowawezesha wahitimu kujiajiri.

Waziri wa zamani wa Elimu na Mafunzo Stadi, Shukuru Kawambwa amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa shule ya msingi ya mchepuko wa kiingereza ya Bright House iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Amesema ili kuondoa changamoto hiyo ni vema kutafutiwa dawa kuanzia watoto wanapokuwa wadogo hadi wanapomaliza vyuo vikuu.

“Nimefurahi kuambiwa shule hii inajenga uwezo wa watoto kujiamini na kujiajiri na sio kuwajengea uwezo kwenye ufaulu pekee,” amesema Kawambwa.

Amehimiza kuwepo kwa ushirikiano kati ya walimu na wazazi ili kujenga kizazi kilicho bora na siyo kuacha mzigo huo kwa walimu peke yao.

“Msiweke nguvu kwenye elimu bora mkasahau kuwalea watoto kimaadili na kiimani,” amesema na kuongeza kuwa watoto wanapaswa elimu inayowajenga kimaadili na kuwa na hofu ya Mungu.

Naye Mkurugenzi wa Shule ya mchepuko wa kiingereza ya Bright House iliyopo Bagamoyo, Profesa Goodluck amesema shule hiyo pamoja na kutoa elimu inayotakiwa, pia inawajengea ujuzi na uwezo watoto wa kujiajiri na kuendesha maisha yao.

Amesema pia inawajengea uwezo wa kuajirika na kuweza kuzalisha na kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi.

“Tunawakaribisha wazazi wafike kuona utaratibu unaotumika wa kufundisha watoto na kujenga kizazi ambacho nchi imekuwa ikitamani kuwa nacho kwa maana ya watu wenye uwezo wa kujiajiri na pia kutengeneza ajira kwa watu wengine.

“Tunawashauri wawekezaji wengine waje wawekeze Bagamoyo kuna fursa na watoto ni wengi, lakini pia waje kujifunza utaratibu tunaoutumia pia kujenga uhusiano mzuri zaidi na serikali na wadau mbalimbali wa elimu ili kuweza kuendesha gurudumu hilo kwa pamoja,” amesema.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hosea Kitunzi amesema shule hiyo mpaka sasa imetimiza miezi nane tokea ilipoanzishwa Januari mwaka huu.

Amesema shule hiyo ilianza na watoto 43 lakini hivi sasa wamefikia 65.

“Sasa hivi kuna changamoto kubwa katika jamii katika habari ya maadili na kujenga watu wanaojiamini wanaokwenda kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ndani ya jamii,

“Tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa tunawaandaa hawa vijana lakini jukumu hili sio letu tu kama shule au kama uongozi tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja kwa maana ya kuwa mwanafunzi aliye bora hajengwi na mwalimu au shule tu hapana,” amesema.

Amesema shule itafanya kazi yake, mzazi kazi yake, jamii kazi yake na serikali pia, wote kwa pamoja ndio atatengenezwa mwanafunzi bora.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button