Msongomano foleni ya malori Tunduma wapatiwa ufumbuzi

MSONGAMANO na foleni ya malori yanayovuka mpaka waTunduma mkoani Songwe imeisha baada ya serikali ya mkoa huo kulishughulikia tatizo hilo kimkakati.

Akizungumza na HabarLEO jana, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael alisema kuisha kwa foleni hiyo hadi ilipofika jana alfajiri kumetokana na kamati aliyoiunda ikiongozwa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani humo.

Dk Michael alisema kamati hiyo pia ilimjumuisha mwenyekiti wa trafiki wa kanda, mkuu wa trafiki mkoa, mwenyekiti wa chama cha madereva wa malori Tanzania na mwenyekiti wa mawakala.

“Kamati hii imekuwa ikizunguka kufuatilia jambo hili na tukakubaliana kuwa baada ya malori yote kuingizwa barabarani kwa wakati mmoja, tukaamua yaingie barabarani kutokana na nafasi ya malori kupita, kwa hiyo tukakubaliana malori ya mafuta yawe yanapita usiku kucha na malori ya makontena na bidhaa za kawaida yapite mchana,” alisema Dk Michael.

Alisema baada ya kukubaliana hilo waliamua kuweka njia mbili ambapo malori ya makontena yanapita kwenye skana wakati magari ya mizigo ya kawaida yalikuwa yanakaguliwa tu na wafanyakazi wa mpakani na malori yanayokwenda DRC yanakaguliwa kwenye mpaka wa Katumbalesa, hivyo hayana sababu ya kupita kwenye skana ya Tunduma.

Dk Michael alisema alizungumza na mawakala wote na kukubaliana kuita malairi 50 au 60 na yakiisha yanaitwa mengine.

Kuhusu mkakati wa kudhibiti foleni alisema kamati hiyo ni ya kudumu na wataiwezesha, lakini serikali ina mpango wa kujenga barabara ya njia nne kutoka Tunduma hadi Igawa mkoani Mbeya, kuna ardhi imetengwa ambayo watailipia fidia ili kujenga yadi za malori ili yasiegeshwe barabarani.

Pia alisema Tanroads wanapasua eneo la takribani mita 800 ili barabara ipite katikati na malori yote yatapita njia hiyo na wataweka mzani kwa ajili ya kupima malori hayo lakini pia TPA watapewa eneo la hekta 500 au 600 ili wajenge bandari kavu kwa ajili ya kuhifadhia mizigo kama makontena.

Mwenyekti wa Kanda wa Chama cha Madereva, Nuhu Mzodoka kupitia video inayosambaa mitandaoni aliishukuru serikali ya mkoa huo kwa ushirikiano waliowapa kwa kumaliza tatizo hilo kwa pamoja.

“Mpaka alfajiri ya leo (jana) foleni ya malori Tunduma imeisha na malori yote yamevuka mpaka kuelekea Zambia.

“Shukrani za dhati zimwendee Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk Francis Michael kwa kuunda kamati iliyoshirikisha kikamilifu viongozi wa madereva na kufanya operesheni iliyomaliza foleni ya watu kukaa wiki nzima na kufanya gari zote zinazovuka kutolala zaidi ya siku moja,” alisema Mzodoka.

Habari Zifananazo

Back to top button