Msusi ashinda zawadi ya gari

Msusi ashinda zawadi ya gari

MAMA wa watoto watatu Easther Norbert anayejishughulisha na kazi ya ususi ameibuka mshindi wa shindano liitwalo Bob Kubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam, Ester Norbert,  baada ya kutangazwa mshindi, ameshukuru kushinda zawadi hiyo ya gari aina ya Toyota IST katika shindano hilo lililoandaliwa maalum kwa wadau wa masuala ya ususi Tanzania.

Mshindi huyo aliyedai ametelekezwa na mumewe na kuachiwa watoto watatu, ambao anawatunza na kuwasomesha mwenyewe kupitia kazi ya ususi amesema ni wakati wa wanawake kusimama imara.

Advertisement

“Nashukuru kwa zawadi ya gari itanisaidia kuwalea na kuwasomesha watoto wangu siamini kabisa,” amesema.

Kwa upande wake Ofisa Masoko wa African Star iliyoandaa shindano hilo, Abubakari Hussen, amesema walianza mchakato wa kupata mshindi kwa miaka miwili na kilichotakiwa ilikuwa ni mhusika kukusanya risiti zilizopo kwenye rasta ili kumpata msusi bora wa mwaka.

Naye msanii Marian Mdee, ambaye ni balozi wa African Star Hair,  amesema anawapongeza wanawake kwa kuwa wapambanaji na kujikwamua na umaskini.