WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya ameeleza alivyopanda vyeo hadi nafasi za juu katika nchi akiainisha mambo makuu yaliyomkabili kuyasimamia baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza kuwa Waziri Mkuu mwaka 1980.
Akizungumza nyumbani kwake katika Kijiji cha Chomvu, Kata ya Usangi wilayani Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, hivi karibuni, alitaja ajenda zilizomshughulisha ni usimamizi wa uzalishaji katika kilimo, ukombozi nchi za Kusini mwa Afrika na ujenzi wa Reli ya Tanzania- Zambia (Tazara).
Alivyopanda vyeo
Msuya alieleza mwaka mmoja kabla ya uhuru, wakoloni walivyoamua kuwachukua Watanganyika wenye elimu, akiwamo yeye, waanze kujifunza kuendesha wizara.
Alisema mwaka 1960, katika kipindi ambacho vuguvugu la kupata uhuru lilipamba moto, alihamishwa kutoka wilayani Pare, akapelekwa Dar es Salaam na kuwekwa kwenye wizara iliyoitwa Serikali ya Mitaa chini ya Waziri Rashid Kawawa na Katibu Mkuu Mzungu.
“Na mimi nilikuwa ni Assistant Secretary (Katibu Mkuu Msaidizi),” anasema na kueleza zaidi: “Zamani mfumo wa wizara ilikuwa Assistant Secretary (Katibu Mkuu msaidizi), Senior Assistant Secretary, Principle Assistant Secretary (Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi), Principle Permanent Secretary (Katibu Mkuu Mwandamizi). Na kwa upande wa hivi vyeo, ni lazima uwe umefanya mitihani. Na ufundishwe jinsi ya kufanya kazi, ambayo siku hizi nafikiri haipo.”
Alisema baada ya muda, shinikizo za kisiasa zilianza na mshauri wa Mwalimu Nyerere (Katibu Mkuu Kiongozi) wakati huo alimshauri kwamba, ripoti wanazopata ni kwamba vijana wanaopelekwa hapo kwenye makao makuu ya wizara wanapaswa watoke nje, waende kwenye mikoa.
“Sasa kama tunawafundisha huku, kule wako wazungu na wahindi, itakuwa na matatizo. Tukaambiwa turudishwe tena huku. Kwa hiyo nikatoka pale nikarudishwa tena Dodoma nikiwa Social and Development Officer Central Province office (Ofisa Maendeleo ya Jamii, Jimbo la Kati).
Jimbo la Kati lilijumuisha Dodoma na Singida ambako walifanya kazi kwa miezi ipatayo tisa na mwaka 1961 wakarudishwa Dar es Salaam katika kipindi ambacho ulishafanyika uamuzi kuwa Tanganyika itapata uhuru.
Anasema Waziri Mkuu, Nyerere na viongozi wa Tanu walitaka wapatikane watu, wajifunze kutokana na kile walichosema kuwa hawana uhakika kama hao makatibu wakuu wazungu waliopo wanawashauri vizuri au la.
Aingia mfumo wa wizara
“Basi tukaingia kwenye mfumo, wakati ule mfumo wa wizara ukaanza ku-take shape (kuchukua nafasi). Mimi niliingia kwenye Idara hiyo ya Maendeleo nikapanda nikawa Kamishna baadaye nikawa Permanent Secretary wa hiyo Wizara ya Maendeleo na Utamaduni,” alisema.
Aliendelea kuteuliwa katika wizara mbalimbali ikiwamo Wizara ya Ardhi, Maji na Makazi; Wizara ya Uchumi na Mipango; Wizara ya Viwanda; Wizara ya Fedha; Wizara ya Viwanda.
Majukumu Uwaziri Mkuu
Msuya alichaguliwa mwaka 1980 kuwa mbunge wa kwanza wa Mwanga na kisha kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.
Akizungumza nafasi hiyo aliyoishika mara mbili kwa marais wawili tofauti, Msuya alisema, “sijui kati yenu kuna mtu aliyesoma katiba yetu vizuri?” alihoji akifafanua kuwa Waziri Mkuu katika katiba, hayuko sawa kama wa Uingereza, au wa nchi nyingine kutokana na katiba kuacha mamlaka yote kwa Rais.
“Waziri Mkuu ni Msaidizi wa Rais na ungeweza kusema ni head prefect (kiranja) wa mawaziri kuhakikisha wanatekeleza kazi zao kwa haraka haraka kutegemea na utashi na uamuzi wa serikali. Hiyo ndiyo kazi kubwa,” alisema.
Alisema hata kwa kuangalia sasa, zaidi waziri mkuu kazi yake ni kusisitiza na kutekeleza yanayotarajiwa, yatekelezwe na wizara mbalimbali kama ilivyoamuliwa na hawezi kubuni lake.
“Maana katiba haikumpa hiyo…na Rais akiteua, kama ni waziri wa elimu, kilimo… ni kumwambia nakupa sehemu hii usimamie na uiendeshe. Na ndio sababu akila kiapo anasema nitamshauri. Awe anamshauri na rais aridhike.”
Ajenda alizosimamia
Akirejelea enzi zake baada ya kushika uwaziri mkuu, anasema ilikuwa mwaka 1980 ambao ulikuwa na tatizo la kiuchumi. Kazi yake ilikuwa ni kushirikiana na viongozi wa mikoani kuona kama wanaweza kuongeza zaidi uzalishaji, zaidi kwenye kilimo.
“Wakati ule, juhudi kubwa zilikuwa kwenye kilimo. Na kilimo hasa cha chakula. Kwa hiyo ndiyo ikatuwezesha kupata hata the big four (mikoa minne ya uzalishaji chakula kwa wingi) ambayo ni Ruvuma, Iringa, Mbeya na Rukwa kwa upande wa uzalishaji wa mahindi na kadhalika,” anasema.
Anasema kazi yao ilikuwa ni kusimamia mfumo wa masoko hususani kwa kujenga barabara. “Wakati huo ndio tulijenga barabara pale Makambako kwenda mpaka Songea,” anasema.
Jambo lingine lililowalazimu kufanya ilikuwa ni kusaidia ukombozi kwa nchi za kusini mwa Afrika hususani, Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na Angola.
“Ajenda hii (ya ukombozi), ilituchukua nguvu nyingi. Rais alikuwa anakwenda kwenye vikao vya Front Line States (nchi za mstari wa mbele) kuona tusaidieje,” anasema. Nchi hizo ni Angola, Botswana, Lesotho, Tanzania, Msumbiji, Zambia na Zimbabwe.
Ujenzi wa Tazara
Anasema ajenda ya ukombozi ilizaa ujenzi wa Tazara baada ya kubainika kuwa wakoloni Rhodesia ya Kusini (Zimbabwe) na Afrika Kusini watazuia bidhaa bandarini kwenda nchi nyingine.
“Na wakizuia, ikawa kazi ya kutafuta namna ya kujenga reli. Nguvu nyingi zilifanyika mpaka hatimaye viongozi wetu, Nyerere na Kenneth Kaunda (wa Zambia) wakaenda kuomba kwa Wachina,” anasema na kuongeza kuwa Wachina walikubali lakini kwa kusema watashirikiana na nchi husika.
Anasema walitumia nguvu na muda mwingi serikalini kusimamia ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi, Zambia. Kwa upande wa Tanganyika (Tanzania), ujenzi uliangukia wizara tatu ambazo ni Wizara ya fedha, Wizara ya Mipango na Wizara ya Ujenzi ambazo zote aliwahi kuwamo.
“Kote huko, (wizara ya) Mipango nilikuwepo kama Katibu Mkuu, Fedha nilikuwa kama Waziri na Katibu Mkuu,” anasema Msuya na kueleza masikitiko ya reli hiyo kutoendeshwa kwa faida.
Septemba mwaka 1965, Serikali ya China, Tanzania na Zambia zilisaini makubaliano ya kujenga reli ya Tazara. China ilitoa mkopo usio na riba, ilisafirisha na kutuma wataalamu wakiwamo wahandisi. Ujenzi ulianza Oktoba, 1970.
Yaliyojiri ujenzi Tazara
Akizungumzia ushirikiano katika ujenzi, Msuya anasema Wachina walisema watasaidia kuleta wataalamu, kuleta vitu ambavyo wanatengeneza kama vile mataruma na reli yenyewe isipokuwa nguvu kazi ambayo ilikuwa ni juu ya Tanzanai na Zambia.
“Na labda hapa nikuelezeni vitu ambavyo vilituaibisha kidogo. Tumefanya hivyo na wao wameshaweka vitu vyao vyote, kwamba hivi vitatoka China …sasa hii local labour (nguvu kazi ya ndani) tunafanyaje?
“Tulipopata hesabu zile za wataalamu wale kwamba tutaingiza kwenye bajeti zetu, ikaonekana kwamba haiwezekani bajeti ya Tanzania au ya Zambia kubeba ule mzigo. Maana fedha hazikuwapo,” anasimulia.
Anaendelea kueleza kuwa walikuwa na vikao kwa takribani wiki mbili mfululizo baina ya Zambia, Tanzania na China. “Sasa kilichokuja kufanyika…kwa ufupi, tulisema tena wachina tupeni fedha za kigeni tulipe watu wetu, wanaofanya kazi. Wachina wakasema, hatuwezi…kama tuna dola zetu tuwaleteeni tugharimie mlipe wafanyakazi wenu, no! (hapana).”
“Na wanatutania wanasema, ninyi mnakaa huko Oysterbay (Dar es Salaam) mara nyingine mnafanya maparty (tafrija) yenu kwenye hoteli na wakati ndio wanajenga kiwanda kama cha Urafiki, na mimi nilikuwa natembelea na wakati mwingine yule mchina…nawaona watu wetu.”
Msuya anasimulia zaidi akisema: Yale mambao yaliyoleta mashine na makaratasi, wao (wachina) wanatandika chini wanalala lakini expert (wataalamu) wetu tunaowaleta, tunawaweka Kilimanjaro (hoteli). Anasema Mchina akasema, “mnaongeza gharama halafu mnasema hamna uwezo?”
Anasema Wachina walisema ingekuwa ni wao, wangetumia majeshi kwa maana ya Jeshi la Wananchi, Jeshi la Kujenga Taifa na Magereza wangefanya kazi hiyo.
Walishauri pia katika maeneo reli inapopita, kila wilaya itoe watu na iwalipe; jambo ambalo lilikuwa gumu. “Kwa hiyo tukakubaliana kwamba, badala yake, Wachina watatoa bidhaa za viwanda vyao, zije ziuzwe kwenye soko letu, zile fedha ndizo zilipie gharama za ndani.”
Anakumbusha kuwa baada ya makubaliano hayo, kilikuwa kipindi ambacho bidhaa mbalimbali kutoka China, ikiwamo chupa za chai, zilimiminika nchini. “Hayo ni baadhi ya mambo ambayo tulikuwa tunafanya,” anahitimisha Msuya.
Wasifu unaonesha mwaka 1960, wakati wa vuguvugu la uhuru, alikuwa miongoni mwa Watanganyika wasomi walioingizwa kwenye mfumo wa wizara wajifunze kuziendesha.
Alifanya kazi kwenye wizara tofauti ama akiwa katibu mkuu au waziri. Nazo ni Wizara ya Ardhi, Maji na Makazi; Wizara ya Uchumi na Mipango; Wizara ya Viwanda; Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda.
Mwaka 1972, akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, aliteuliwa kuwa mbunge na kupewa uwaziri wa wizara hiyo. Mwaka 1975, Nyerere alimteua tena kuwa mbunge na kumpa uwaziri wa viwanda aliotumikia hadi mwaka 1980 alipokuwa mbunge wa jimbo la Mwanga mkoani Kilimanjaro na kisha kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu.