Msuya: Ndoto za Nyerere zimetimia

WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Cleopa Msuya amesifu ndoto za Mwalimu Julius Nyerere zinavyotimizwa kupitia miradi mbalimbali.

Ametaja baadhi ya miradi hiyo likiwamo Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na kueleza alivyoushughulikia akiwa waziri na sababu za kutotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Akipongeza uthubutu wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya John Magufuli kutekeleza mradi huo wa umeme, Msuya anaeleza alivyofanya utafiti wake akiwa Waziri wa Fedha na Mipango na ambavyo serikali ilisaidiwa na Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) kufanya kila kitu mpaka hatua ya kwenda kwenye zabuni.

“Hydroelectric scheme hii ya Nyerere au Stigler’s Gorge, mimi nakumbuka ile nilifanya study (utafiti) wakati nikiwa Waziri wa Fedha na Mipango. “Tulisaidiwa na wa Norad (Shirika la Maendeleo la Norway) wakafanya kila kitu mpaka hatua ya kwenda kwenye tender(zabuni),” anasema.

Msuya ambaye alihudumu katika Wizara ya Fedha tangu mwaka 1970 hadi 1972, anasema kilichokwamisha mradi huo ni kwamba, kiasi cha umeme ambacho ilibidi kizalishwe, kisingeweza kuuzika kutokana na uchumi wa nchi ulivyokuwa.

“Sasa tunafika huku upande wa pili, umeme unazimika kila siku. Akasema (Magufuli) mimi nalijaza hili (bwawa),” anasema Msuya na kueleza kuwa ili nchi isonge mbele inahitaji uongozi bora. Alieleza kufurahishwa na ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan ameendeleza mradi huo akisema, “kwa hilo, Rais wa sasa amefunga lile lango na wametuambia mwaka ujao wa 2024, umeme utatoka.

“Ninachotaka kukuambia ni kwamba, hii nchi ili isonge mbele inahitaji uongozi.” Anatoa mfano wa China na Korea Kusini zilivyosonga mbele kiuchumi kutokana na kuwa na uongozi usioyumba. “Wakati tunanegotiate(jadiliana) mambo ya reli (Tazara), nilikwenda China. Wale watu walikuwa wanalala chini na vitanda vyao kama vile vya kwetu vya kamba, ukienda kijijini unapewa unalala.

Sasa hivi China inashika nafasi ya pili duniani kwa uchumi baada ya Amerika…kwa nini? Communist (chama) imeshika madaraka na kuwatawala wale viongozi, haiyumbi.” Anasema pia alipokwenda Korea Kusini kabla ya Tanganyika kupata uhuru, nchi hiyo hawakuwa mbali na ilivyokuwa hapa nchini. “Siku ile natoka pale narudi nyumbani, nimepita Japan, wakapindua serikali. Alichukua mwanajeshi anaitwa Park Chung-hee. Huyo Park ndiye aliyeleta mapinduzi Korea Kusini.”

Anasimulia kuwa Park alisomesha watu kwa ajili ya viwanda alivyotaka, akaisimamia hatimaye nchi imeingia imeingia kwenye Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) inayojumuisha nchi 36 zilizoendelea.

Anaitaja pia Vietnam kuwa ni nchi iliyopigwa vita na mataifa mbalimbali lakini baada ya hapo, inapanda haraka na sasa ni mzalishaji mkubwa wa chai, korosho na hata katani. Sababu anayotaja ni kutoyumba kwa chama.

Kwa upande wa Tanzania, Msuya anasifu mfumo uliowekwa na chama cha Tanu, CCM, Mwalimu Nyerere, mkakati wa viwanda na hata Azimio la Arusha ambao anasisitiza kuwa ili uende vizuri, unapaswa kupata uongozi bora.

Amsifu Magufuli “Vitu hivi unataka upate mtu ashike kwa muda mrefu ili muende. Kwa mfano, Magufuli (Mungu amuweke mahali pema peponi), huyu kama si yeye aliyekuja akasema; hii miradi, anaiita ya kimkakati na nitaitekeleza, imetekelezeka.”

Anataja miradi mingine ambayo Serikali ya Awamu ya Tano ilifanya vyema ni pamoja na kuhamia Dodoma mpango uliokuwapo tangu wakati wa Mwalimu Nyerere. Mradi mwingine wa kimkakati ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao Msuya anakumbusha jinsi walivyowahi kuletwa wawekezaji wakashindwa.

“Tulipanga kuleta Wahindi wawe chini ya Tanzania Railway Cooperation wakawa wanababaisha babaisha, wanachukua vifaa vyetu. Yeye akasema hapana nitafanya hivyo…ndege zimetushinda, mpaka wakati fulani walikuwa wakisema, tunashindwa na nchi ndogo kama Rwanda. Sasa angalia tuna ndege kama sita au saba,” anasema.

Waziri Mkuu huyu mstaafu anaweka bayana kuwa katika mapinduzi haya, yapo mambo ambayo Magufuli alichukua yasiyoelezeka. “Unajua ukitaka kuleta mapinduzi, ndio sababu under normal circumstances kwenye serikali za kistaarabu unaita state of emergency (hali ya dharura). “…unanyima watu haki fulani ili kama ni vita au nini, ili mshinde. Sasa vitu vingine alivyovifanya Magufuli ni kama vya state of emergency, kutumbua watu; kuonesha kwamba tunapoteza fedha nyingi hapo bandarini, tunalipa watu hewa…” Anasifu pia eneo la madini ambalo Magufuli alizuia makinikia kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Kwa hiyo, unahitaji kuwa na awamu inaitwa, kama ni vita, inaitwa state of emergency …. kipindi hiki tunachopita haki za binadamu nyingine zitadhulumiwa kwa sababu tunataka kufanya hivyo… Sasa labda yeye alifanya bila kutamka hilo.” Kwa mujibu wa Msuya, nchi zote zinazoendelea zimefanya hivyo.

Anatoa mfano wa Singapore na Serikali ya Dubai akisisitiza, “kama mnataka kujua zaidi soma kitabu chao …‘fishing village’ (kijiji cha uvuvi) … ndogo kuliko hata Bagamoyo. Sasa ni giant. Kwa nini? Ni mtu mmoja, anaitwa yule Shehe (Kiongozi wao Mohamed Rashid Al Maktoum) anaamua, na kama mambo hayafanyiki anafukuza watu.

Na hii ni ili kitu kionekane.” Hata hivyo, Msuya anasema ili kiongozi afanye makubwa, panahitajika kuwapo mfumo na lazima chama kimuunge mkono ili mambo yaende bila kujali kama kiongozi husika yupo au la. “…mimi nimemtaja Magufuli kwa sababu alionesha uwezo. Lakini cha muhimu ni kwamba, lazima awe backed (aungwe mkono) na chama ambacho ama Magufuli yupo au hayupo, bado msimamo utabaki palepale,” anasema.

Ushiriki sekta binafsi Msuya ambaye anatajwa kuwa ‘baba wa viwanda’, anasema serikali kushirikiana na sekta binafsi si jambo la ajabu wala geni. Anakumbushia alipokuwa serikalini alivyokuwa wa kwanza kupeleka mapendekezo kuhusu ushirikiano na sekta binafsi kuboresha kiwanda cha bia na cha sigara. Anasema miaka fulani baada ya uwekezaji huo, “kampuni ya bia ilipongezwa kwa mafanikio ikiwamo ulipaji mkubwa wa kodi… lakini sasa hapo katikati ikaja wa kusema uzeni tu,” anasema na kueleza masikitiko kuhusu uuzwaji wa viwanda vingi ikiwamo cha Kiwanda cha Zana za Kilimo cha Ubungo (UFI).

Watendaji serikalini Akizungumzia utoaji nafasi za uongozi serikalini, Msuya anashauri uwepo mfumo wa uchaguzi ambao utawezesha kuwaingiza vijana wenye ujuzi wanaoweza kusukuma shughuli za maendeleo. Anashauri wawekewe mazingira ya kufanya kazi bila kuingiliwa kusiko kwa lazima ili waelewe kuwa wameaminiwa.

“Mimi kwa mfano, wakati sijawa waziri mkuu, nilikuwa waziri chini ya Mwalimu Nyerere na chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Niliji feel free. Nilipewa uhuru wa ajabu sana. I only went to them (niliwaendea pale tu) kama ninaona jambo linanihangaisha.” “Otherwise (vinginevyo) wanasema, kama umeelewa ninacholenga, nenda, fanya kazi. Sasa hivi naamini wapo watu wanaofanya hivyo.

Kwa hiyo mimi naamini sisi tulikuwa na bahati, rasilimali ndio hazikuwapo. Lakini kama ndio hamkulisimamia vizuri mnaweza kunyang’anywa,” anasema Msuya akilinganisha enzi zake na sasa juu ya uwapo wa rasilimali za kuinua maendeleo.

Habari Zifananazo

Back to top button