DAR ES SALAAM:: WAZIRI Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amesema pamoja na mapungufu ya hapa na pale, Tanzania inapaswa kujivunia namna nchi inavyoendeshwa kwa Utawala wa Sheria, ikihusisha pia utiifu na heshima juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari, kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Msuya amesema hili linajidhihirisha katika namna viongozi wa ngazi za juu wanavyoachiana madaraka kwa utulivu na amani huku wakirejelea katiba inasema nini.
“Kwa mfano Mzee Mwinyi alivyochaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano baada (hayati) Nyerere. Lakini hivi karibuni baada ya kifo cha (hayati) Magufuli ‘automatically’ naibu wake ambaye alikuwa Mama Samia alichukua hatamu ya uongozi bila mtikisiko wowote,” amesema kiongozi huyo mstaafu.
Amesema ingelikuwa ni nchi nyingine (bila kutaja majina) jambo kama hili lisingeliwezekana, vita ingelitokea.
“Na hasa kama ni mama. Lakini ilimradi katiba imeandikwa hivyo, wakamwita, akaapishwa na yeye akachukua hatua za kikatiba kupata Makamu wa Rais,” amesema mstaafu huyo.
Amesema, Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuchukua hatamu ya uongozi amefanikiwa katika kuonesha kuwa jinsi si chochote katika uongozi badala yake Rais ni Taasisi.
“Kupitia maelezo yake yenye nguvu ‘strong statement’ ya Rais kuwa ‘Mnayemuona hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano sio Mama’,” amesema Msuya.
Amesema, kauli ile ilionesha namna alivyo imara. Pia kupitia kuendeleza miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na mtangulizi wake na kuongeza mingine inaonesha namna alivyofanikiwa katika uongozi wake.