Mtafiti SUA na mkakati kuongeza uzalishaji maharage

DAR ES SALAAM; INAELEZWA kuwa walaji wengi wa maharage hapa nchini, hupendelea kutumia aina mbili ambazo ni soya njano ama njano golori na soya kijivu ama kablangeti.

Kupendwa kwa maharage hayo na walaji kumemfanya Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Luseko Chilagane kuyafanyia utafiti uliolenga mbegu bora zenye ukinzani wa ugonjwa wa doa pembe na zenye sifa zinazopendwa na walaji.

Dk Chilagane ambaye yupo katika Idara ya Sayansi ya Mimea Vipando na Kilimo cha Bustani, anasema ni mnufaika wa sh milioni 70 ambayo ni fedha ya serikali kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Advertisement

Anasema: “Mradi wangu ulihusisha ugunduzi wa aina bora za maharage ambazo zitakuwa na ukinzani wa magonjwa, lakini niliangalia ugonjwa mmoja wa msingi ambao unaitwa ugonjwa wa doa pembe unaosababishwa na vimelea vya fangasi.”

Maelezo yake ni kwamba, ameangalia faida ambazo zinapatikana kwenye maharage yanayoitwa maharage ya kienyeji kwa kuzingatia mbegu ambazo wakulima wanazilima.

“Lakini pia nilitaka kuhamisha ukinzani wa ugonjwa huu kutoka kwenye maharage mama ya kienyeji ambayo yana vinasaba kwa ajili ya kukinzana na ugonjwa nivipeleke kwenye maharage yanayopendwa na wakulima na walaji nchini,” anasema na kuongeza kuwa ukienda masoko yote utayakuta hayo maharage na ndiyo yanauzwa bei ya juu zaidi.

Anauelezea ugonjwa huo wa doa pembe kuwa unasabisha madoadoa kwenye majani yanayoondoa ile kijani ya kwenye majani, ambayo ndiyo inasababisha utengenezaji wa chakula na mbegu, wakati mbegu ndizo maharage kama chakula kwa mlaji.

“Kwa hiyo ugonjwa ukiingia ukisababisha upungufu wa hii kijani maana yake inasababisha upungufu wa mazao. Kwa hiyo ukiweza kudhibiti ugonjwa huu unaongeza hii sehemu ya kijani ili kuongeza pia uzalishaji.

“Ugonjwa huu unashambulia sana maharage kwenye sehemu za baridi na sehemu zenye unyevunyevu, ambapo ukiangalia ndizo sehemu ambazo tunazalisha maharage kwa sana,” anasema.

Anasema ugonjwa huo ni wa msingi sana kuufanyia kazi kwa kuwa maeneo mengi yanayozalisha maharage ndiyo yenye baridi ukiwemo Mikoa ya Mbeya, Arusha na Morogoro eneo la Mgeta.

“Kwa hiyo katika mradi wangu nilifanya utafiti na nilitengeneza mbegu hazijafikia hatua ya mwisho wa kuitwa mbegu, lakini zipo kwenye hatua fulani ya mchakato wa kuendelea kuwa mbegu baadaye, ambazo zina ukinzani wa huu ugonjwa na nilitengeneza ukinzani ili pia ukinzani huu uingie sokoni ziwe kati ya zile mbegu ambazo zinapendwa,” anasema.

Anaeleza kuwa mbegu nyingi zinazotengenezwa na kuitwa mbegu bora zinaishia kwenye makabati hazifiki kwa wakulima, ndio maana katika utafiti wake alichukua mbegu inayopendwa na wakulima ili aweke hicho kinasaba kwenye hiyo mbegu yao, ambapo sifa nyingine zitabaki kama wanavyozitaka, ila atakuwa ameongeza kinasaba kwa ajili ya ukinzani wa ugonjwa.

“Sasa ninazo jumla ya aina 18 na zina wazazi tofauti tofauti katika hizi kuna ambazo zina ukinzani wa huu ugonjwa wa doa pembe.

“Lakini kuna nyingine ambayo niliitengeneza maalum kwa ajili ya kuunganisha hivi vitu ambavyo walaji wanapenda kutoka kwenye soya njano na kutoka kwenye kijivu nikaziunganisha nikaweka kwenye mbegu moja.

Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk Luseko Chilagane akionesha sampo ya maharage kwa watafiti  kutoka Costech, walipotembelea moja ya maabara chuoni hapo. Wa kwanza kulia kwa mtafiti ni Dk Bunini Manyilizu na anayemfuatia ni Dk Deogracious Protas. (Picha zote na Lucy Ngowi).

“Kwa hiyo hii mbegu moja tunategemea itakuwa na sifa ambazo zitaunganisha ile ya kutoka kwenye kijivu na ile ya kutoka kwenye soya njano ambayo ninaamini kwa sababu hii ndiyo inapendwa zaidi, naamini itakapofika mwishoni itachukuliwa na wakulima kwa urahisi zaidi,” anasema.

Anasema utafiti upo katika hatua za uainishaji wa sifa za maharage hayo yaliyoboreshwa na uchaguzi wa yale yatakayofanya vyema kwenye mazingira ya mkulima.

Utafiti na uchaguzi wa awali umefanyika SUA na kupatikana aina tofauti 18 ambazo ndio zitapelekwa kwenye mazingira ya mkulima,  ili kuhakiki sifa za maharage hayo, hasa ukinzani wa ugonjwa huo, sifa pendwa kwa walaji na ongezeko la mavuno kabla hayajaidhinishwa kuwa mbegu bora na kuanza kutumika na wakulima.

Anaeleza kuwa kabla ya uboreshwaji maharage hayo hayafikishi hata tani moja kwa hekari ambapo inategemewa baada ya uboreshwaji uzalishaji utafikia kuanzia tani moja na nusu mpaka tani tatu kwa hekari.

Kwa maelezo yake amesukumwa kufanya utafiti huo baada ya kutembelea masoko na kukuta kuna mbegu nyingi za maharage, lakini sokoni zipo aina ya kijivu na njano pekee.

Anasema alijiuliza ni kwa nini mbegu hizo mbili tu zipo sokoni, majibu aliyoyapata ni kwa kuwa zina sifa zinazopendwa na walaji pamoja na wakulima.

Anaeleza pia utafiti wake utakapokamilika utawezesha kuongeza uzalishaji kwa wakulima kwa kuwa hivi sasa wakulima wanapata kilo 900 kwa hekta ambayo ni ndogo sana, lakini kwa kutumia mbegu hizo zilizofanyiwa utafiti mavuno ya wastani yanayotarajiwa ni kuanzia tani moja na nusu kwenda juu

Kuhusu maharage pendwa hayo, Mratibu wa maharage nchini kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga mkoani Mbeya, Reinfrid Maganga anaungana na mtafiti kutoka SUA kuwa maharage hayo yanapendwa kwa kuwa ni matamu pia yana gesi kidogo.

“Tuna aina moja ya maharage ya kijivu au yanajulikana kama kablanket, kwetu TARI yanajulikana kwa jina la Uyole 18, Na aina mbili zipo katika hatua za mwisho za kukamilika,” anasema na kuongeza kuwa maharage ya njano goroli wanaitambua kwa jina la selian 13.  Costech ni mshauri mkuu wa serikali katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia na ubunifu.

Katika kufuatilia na kujua matokeo ya fedha za serikali zinazotolewa na tume hiyo, watafiti kutoka Costech wamekuwa wakitembelea miradi mbalimbali ili kuona jinsi inavyoleta matokeo chanya kwa jamii.

Meneja Uhifadhi Taarifa na Machapisho kutoka tume hiyo, Dk Philbert Luhunga anasema ni vyema jamii ikajua tafiti na bunifu zinazoleta matokeo chanya ili iweze kuzitumia.