Mtanzania atikisa tuzo za AKMA 2022

WASHINDI 15 wa tuzo za Muziki za Aga Khan 2022 (AKMA), akiwemo mtunzi wa nyimbo za dini kutoka Tanzania, Yahya Hussein Abdallah, wamekabidhiwa kitita cha Dola za Kimarekani 500,000, takribani Sh bilioni 1.16.

Mbali na shughuli zake za kimuziki, mkazi huyo wa Dar es Salaam ni msomaji maarufu wa Qur’an.
Sherehe ya kuwakabidhi tuzo washindi hao zilifanyika Muscat, Oman hivi karibuni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na AKMA, mbali na kiasi hicho cha fedha, washindi hao watapata kazi kutunga nyimbo mpya, kupewa mikataba ya kurekodi na usimamizi wa wasanii, kuungwa mkono katika miradi ya elimu, na ushauri wa kiufundi au usimamiaji wa miradi ya uhifadhi, utunzaji na usambazaji wa muziki.

Mtanzania huyo ameelezewa kuwa ni mwanamuziki anayeweza kutunga na kuimba kwa Kiswahili na baadhi ya lugha mahalia 126 zinazopatikana Tanzania.

Awali, washindi wa tuzo hizo walitambuliwa huko Geneva, Uswisi mnamo Oktoba 6, 2022 kwa juhudi zao za kuzungumzia masuala ya sasa ya kijamii na mazingira huku wakidumisha na kuendeleza mapokeo ya kimuziki.
Tuzo hizi ambazo hufanyika kila baada ya miaka mitatu zilianzishwa na Mtukufu Aga Khan mwaka 2018, kwa lengo la kubaini ubunifu wa kipekee, kipaji na biashara katika muziki kwenye jamii mbalimbali diniani, ambazo Waislamu wapo kwa wingi.

Kwa mujibu wa AKMA, tuzo za Muziki za Aga Khan zinaakisi imani ya Mtukufu Aga Khan, Imamu mrithi wa 49 wa Waislamu wa Ismaili kwa maono kuwa muziki unaweza kutumika kama nguzo ya utamaduni, ambayo inaimarisha hali ya mtu kujiona sehemu ya jumuiya, utambulisho na urithi na wakati huo huo ukiwafikia kwa nama iliyo madhubuti watu wa tamaduni nyingine.

Wakati wa kutangaza washindi, Jopo la Majaji wa Tuzo hizi lilionesha shauku ya kuwaunga mkono wagombea wengi kadri iwezekanavyo kati ya wanamuziki 400 kutoka nchi na tamaduni mbalimbali iwapo kutatokea uhitaji wa haraka wa wanamuziki na waelimishaji wa muziki.

Pamoja na kutoa mchango wao katika uhifadhi na udumishaji endelevu wa urithi wa muziki, washindi wengi miongoni mwao wanatumia nguvu ya muziki kukuza uelewa wa masuala ya kijamii na mazingira.

Washindi wengine ni pamoja na Zakir Hussain (India), Afel Bocoum (Mali), Asin Khan Langa (India), Coumbane Mint Ely Warakane (Mauritania) na Daud Khan Sadozai (Afghanistan).

Wengine ni Peni Candra Rini (Indonesia), Soumik Datta (Uingereza), Yasamin Shahhosseini (Iran), Zarsanga (Pakistan), Dilshad Khan (India) na Golshan Ensemble (Iran).

Mbali na wanamuziki hao, washindi wengine ni Sain Zahoor (Pakistan), Seyyed Mohammad Musavi na Mahoor Institute (Iran) pamoja na Zulkifli & Bur’am (Aceh, Indonesia).

Habari Zifananazo

Back to top button