JAJI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman anaongoza ujumbe wa majaji na wataalamu wa sheria wa Afrika (AJJF) kufuatilia namna Mahakama Kuu nchini Kenya inavyosikiliza shauri la kupinga matokeo lililowasilishwa na mgombea wa urais kupitia Muungano wa Azimio, Raila Odinga.
Ujumbe huo akiwemo Jaji Lillian Tibatemwa kutoka Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Ivy Kamanga kutoka Mahakama ya Rufaa ya Malawi, Jaji Moses Chinhengo kutoka Mahakama ya Rufaa ya Lesotho na Jaji Henry Boissie kutoka Mahakama ya Afrika Kusini uliwasili Nairobi Jumatatu.
Taarifa iliyotolewa jana na jukwaa hilo kwa vyombo vya habari ilisema majaji hao watahudhuria katika vikao vyote vya kusikiliza shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi pamoja na kuandaa ripoti kuhusu mwenendo mzima wa shauri hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waangalizi hao watakuwa na jukumu pia la kuangalia uhuru wa Mahakama katika kutoa haki kwa kuzingatia viwango vya kimataifa na haki za binadamu.
Waangalizi hao pia watatakiwa kuchunguza mazingira ya kijamii na kisiasa yanayozunguka katika utoaji wa haki ambapo mwisho watatakiwa kuandaa ripoti itakayoonesha mwenendo mzima wa shauri mahakamani na jinsi Mahakama ilivyokuwa huru katika maamuzi yake.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa waangalizi hao watakutana kwa mashauriano na wakuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Mkurugenzi wa Mashtaka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya shauri hilo kuanza kusikilizwa ambapo Mahakama ina hadi Septemba 5 kuweza kutoa maamuzi yake.
Wiki iliyopita Odinga aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kenya la kupinga kutangazwa Dk William Ruto kuwa Rais Mteule wa taifa hilo kupitia Uchaguzi Mkuu uliofanyika Agosti 9, mwaka huu.
Katika wasilisho la hoja za kisheria lenye kurasa 70, mwanasiasa huyo anadai kuwa kulikuwa na juhudi zilizopangwa mapema za kubadili matokeo ya uchaguzi huo.
Jopo la mawakili wa Odinga 46 wakiongozwa na Wakili James Orengo na Wakili wa Muungano wa Azimio, Daniel Maanzo, waliwasilisha malalamiko hayo kwa njia ya mtandao katika Mahakama ya Milimani iliyopo Nairobi, kabla ya muda wa mwisho kikatiba ambao ni siku ya saba tangu matokeo kutangazwa.
Katika maombi yao, mawakili hao wanaiomba mahakama kumwamuru Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, George Kinoti kutoa taarifa, picha, ripoti, vifaa kompyuta mpakato na simu na vifaa vingine vinavyohusishwa na uchaguzi.
Pia mahakama imuamuru Kinoti awasilishe kompyuta mpakato iliyochukuliwa kutoka kwa Wakala wa Chama cha UDA, Koech Geoffrey na pia kuitishwa kwa uchaguzi mpya ambao hautakuwa chini ya Mwenyekiti wa sasa wa IEBC, Wafula Chebukati pamoja na kupitiwa upya kwa fomu za matokeo za 34A, 34B na 34C.