Mtaturu: Dk Slaa amepoteza mwelekeo

MBUNGE wa Singida Mashariki (CCM),Miraji Mtaturu amemjibu aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk.Wilbroad Slaa kuwa amepoteza mwelekeo baada kukosa nafasi serikalini.

Kauli hiyo ameisema katika mkutano wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo katika jimbo hilo ikiwa ni kuendelezo wa ziara yake mkoani Singida ya kukagua uhai wa chama mashinani na kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2020/25.

Hivi karibuni Dk Slaa aliibuka katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilayani Karatu,mkoani Arusha akikashifu CCM na kusema katiba mpya ni lazima na inapaswa isiwatambue Wakuu wa Wilaya.

Advertisement

Kutokana na kauli hizo,Mtaturu amesema Dk Slaa ni bora awe mzee mwenye busara atulie baada ya kukosa nafasi serikalini kwa sasa na sio kukashifu chama.

“Kuna umuhimu wakuu wa wilaya kuendelea kuwepo kwenye katiba na hii ni kutokana na umuhimu wao katika kusimamia maendeleo ya wilaya,amesema Mtaturu.

Amesema hivi sasa Watanzania wanataka kusikiliza hoja zenye mashiko na maendeleo na sio porojo.

“Hapa jimboni nilipoingia tulikuwa nyuma kimaendeleo tangu mwaka 2018 lakini sasa hali imebadilika kila kata na kijiji vyote vina miradi ya shule, hii inaongeza imani kwa wananchi na ndio maana leo wanachama wa vyama vingine wanavihama na kurudi CCM baada ya kuona maendeleo kwa vitendo na sio porojo,”amesema Mtaturu.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *