Mtemvu alia kukosekana kadi za elektroniki

Aitaka Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi kuendeleza Mshikamano

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Mkoa wa Dar es Salaam  Abbas Mtemvu amelia kukosekana kwa kadi za Elektroniki za Chama hicho kitu ambacho kinafanya kupoteza wanachama wengi.

Akifungua mafunzo ya siku tatu ya Uongozi wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi  ya CCM Mkoa  wa  Dar es Salaam, leo Januari 12, 2022 Mtemvu amesema yeye binafsi ameomba kadi huu mwaka wa pili lakini hajapata.

“Wanachama wengi wanataka kadi lakini hawana, kuna watu wengi wanataka kujiunga CCM lakini changamoto ni kadi, tarehe 14 tunakikao cha Halmashauri Kuu Taifa, nitalifikisha kwa namna yangu jambo hili kwa Rais Samia Suluhu Hassan Mwenyekiti wetu wa chama.” Amesema
Aidha, Mtemvu amewataka vongozi wa Kamati ya Utekelezaji wa CCM Dar  kuendeleza nidhamu,  mshikamano na ushirikiano ili kuhakikisha kazi ilani ya  CCM inatekelezwa  ili wanachama na wananchi kwa ujumla waendelee kuwa na imani na Chama hicho.
Amesema kuna umuhimu wa viongozi wa chama hicho kuhakikisha kamati ya Siasa kutoa hamasa kwa wanachama na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha Chama hicho kinafanya vizuri katika chaguzi zijazo.
Pia,  amewataka viongozi hao kushuka kwenye kata, wilaya na matawi kutoa elimu kuhusu masuala ya chama hususani ilani ya  CCM  na utekelezaji wake katika maeneo mbalimbali kwenye Mkoa wa Dar es Salaam.
Nae, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam Adam Ngallawa ameitaka kamati hiyo  kuhakikisha wanatumia michango kutekeleza miradi mbalimbali ili Juhudi za Jumuiya ya Wazazi zionekane na wanachama kuwa na imani na chama hicho.
Aidha, amewataka viongozi wa kamati ya utekelezaji kuwa kiungo kwa wazazi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwa wananchi wa mkoa  huo kwani ndani yao wamo vijana na wanawake, hivyo wametakiwa kuhakikisha Chama kinakuwa imara.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salam,  Khadija Ally amesema wamejipanga kikamilifu kufanya vizuri kwenye kuelekea chaguzi zijazo mwakani 2024.
Amesema, kwa kuwa amechaguliwa kwa kuaminiwa hatahikikisha anatoa ushirikiano wa kutosha katika  utekelezaji wa ilani ya  chama hicho na ndio maana wakaona kuna umuhimu wa kupata mafunzo ya uongozi ili kila mmoja ajue mipaka yake.

Habari Zifananazo

Back to top button