Mtibwa, Geita zatakata Ligi Kuu

Mtibwa, Geita zatakata Ligi Kuu

TIMU za Mtibwa Sugar na Geita Gold zimetakata katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushinda na kuondoka na pointi zote tatu jana.

Mtibwa Sugar wenyewe waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani mkoani Morogoro.

Mtibwa Sugar walianza kufunga bao la uongozi dakika ya pili lililofungwa na mshambuliaji, Adam Adam dakika ya pili ya mchezo na kuwapatia uongozi wenyeji.

Advertisement

Coastal Union walisawazisha bao dakika ya 13 lililofungwa na mshambuliaji, Mubarack Amza na kufanya matokeo kuwa 1-1, Mtibwa Sugar waliongeza bao la pili katika dakika ya 32 lililowekwa kimiani na kiungo Juma Nyangi.

Matokeo hayo yameifanya Mtibwa Sugar kufikisha pointi 15 na kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakati Coastal Union wao wakibaki katika nafasi 11 na pointi zao 12.

Nao Geita Gold wametakata ugenini baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Mabao ya Geita Gold kwenye mchezo huo yalifungwa na Yusuph Kagoma katika dakika ya 34, Danny Lyanga dakika ya 38, Shown Oduro dakika ya 58 na Edmond Johns dakika ya 71 wakati mabao ya Tanzania Prisons kwenye mchezo huo yalifungwa na Oscar Paul dakika ya 11 na Oduro akijifunga dakika ya 46.