MTOTO Robert Maganga (2) amefariki dunia baada ya kutumbukia katika shimo lililokuwa limechimbwa na wazazi wake kwa ajili ya kuvuna maji jirani na nyumba yao katika Kijiji cha Ngogwa, Manispaa ya Kahama.
Akizungumza na HabariLEO jana katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, baba mzazi wa mtoto huyo, Gabriel Robert alisema majira ya saa mbili asubuhi alikuja mteja wa kuchimbiwa mihogo shambani na yeye alikwenda kumhudumia.
Gabriel alisema marehemu alikuwa akimfuata mama yake aliyekuwa akivuna mahindi shamba jingine lakini katikati ya shamba hilo lipo bwawa ambalo lilichimbwa takribani miaka 10 iliyopita kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
“Lakini marehemu akiwa na watoto wenzake wawili mmoja akiwa na miaka miwili na nusu na mwingine miaka mitatu walikuwa wakimfuata mama wa marehemu na kushindwa kuvuka na matokeo yake watoto wawili wakadumbukia kwenye bwawa lililokuwa na maji,” alisema Gabiriel.
Alisema mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu hakuingia kwenye bwawa hilo alivyoona wenzake wameshindwa kutoka akakimbia kwenda kuwaita wakubwa ndipo walipowaokoa na kukimbizwa hospitalini lakini Maganga alifia njiani na mwingine ni mahututi baada ya kunywa maji na tope.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Sophia Shabani alikiri kuwapokea watoto hao ambapo mmoja alilazwa na kuendelea kupatiwa matibabu na kwamba wa pili alifikishwa hospitalini hapo akiwa amekwishafariki na mwili wake umehifadhiwa.
Diwani wa Kata ya Ngogwa, Kamuli Mayunga alisema watoto wanatakiwa kupata ulinzi na usalama wa kutosha na aliwashauri wananchi wote wenye mabwawa au mashimo karibu na nyumba zao kuyawekea uzio ili kuepusha vifo visivyo vya lazima kwa watoto wadogo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Leonard Nyandahu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.