Mtoto ajinyonga akibembea kwenye mwembe

MTOTO wa miaka sita aliyetambulika kwa jina la Tumaini Emmanuel, amekufa kwa kile kinachodaiwa kujinyonga kwa bahati mbaya kwenye mti wa mwembe wakati akibembea.

Tukio hilo lilijiri katika Kijiji cha Ndurumo, barabara ya nne katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi.

Inadaiwa kuwa mtoto huyo alikuwa nyumbani kwao na ni kawaida yake kucheza kwenye mti huo akifunga kamba juu ya mti na kuanza kubembea.

Wakati tukio hilo likitokea, wazazi wake walikuwa shambani na hakuna mtu yeyote aliyekuwa karibu na nyumba yao ili kumwokoa zaidi ya pale wapita njia walipoona mwili wake ukiwa juu ya mti akiwa tayari keshakufa.

Wakizungumzia kifo cha mtoto wao, wazazi walisema taarifa hizo wamezipata wakiwa shambani kwa kuwa nyumbani alibaki mtoto huyo aliyepoteza maisha pamoja na dada yake.

“Mimi sikuwapo nyumbani, mtoto alikwenda kujining’iniza kwenye kamba hapo juu ya mwembe, alikuwa anabembea, nimesikia alikuwa amejifunga kamba shingoni,” alisema baba wa mtoto huyo, Emmanuel Kagoma.

“Hapakuwa na ugomvi wowote, alikuwa akicheza na inaonekana alifunga kamba moja juu ya mti, sasa wakati akibembea aliingiza shingo kwenye kamba huku miguu ikiwa chini… Basi ndiyo hayo yakatokea,” alieleza mama wa mtoto huyo, Juliana Kiana.

Majirani walisema matukio kama ya kujinyonga wamezoea kuyasikia kwa watu wazima na siyo kwa watoto kama ilivyotokea katika familia hiyo, hivyo wameshangazwa na tukio hilo.

“Tukio hili tumelipokea kwa mshangao kwa kweli, sababu mtoto alikuwa mdogo ambaye hawezi kufikia uamuzi wa kujinyonga na ndio maana tunasema ilikuwa ni bahato mbaya. Alijinyonga katika michezo sawa na watoto wanaoiba bastola ya baba na kujipiga risasi bila kujua,” alisema jirani mmoja bila kutaka jina lake litajwe gazetini.

Jirani mwingine alisema: “Katika hali ya kuulizia, tumeambiwa mtoto alikuwa akipenda sana kuchezea hapo akitumia kamba kama bembea. Tunachohisi, kwa kuwa alikuwa peke yake aliona hana mtu wa kumsukuma katika bembea, hivyo akahisi kwamba atakapoweka ile kamba shingoni atabembea kwa urahisi.”

 

Habari Zifananazo

Back to top button