Mtoto aliyeibwa apatikana, mwizi abambwa
BAADA ya kuripotiwa wizi wa mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi saba Desemba 20, mwaka huu katika wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, hatimaye mtuhumiwa aliyemwiba mtoto huyo amekamtwa na Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wibroad Mtafungwa alisema mama wa mtoto huyo, Salma Athuman (34), alimwachia mtoto mke wa mtoto wake aitwaye Martha Paulo (25) na kwenda katika shughuli zake.
Alisema Salma aliporudi nyumbani siku ya tukio hakumkuta mtoto wake na hakuwa na wasiwasi kwa kuwa alijua mtoto wake yuko kwenye mikono salama kwa mkamwana wake, Martha.
Alisema lakini muda ulizidi kwenda bila ya kumwona mwanae na alipojaribu kumtafuta Martha pia hakufanikiwa kumpata hata kwa njia ya simu na ndipo alipoamua kwenda kutoa taarifa polisi.
Alisema baada ya taarifa hiyo kutolewa upelelezi na msako mkali ulifanyika na ilipofika Desemba 22, mwaka huu katika Kata ya Nyankumbu, Geita mjini, polisi walifanikiwa kumkamata Martha akiwa na mtoto huyo.
Alisema mtuhumiwa alikutwa akiwa amejificha nyumbani kwa wifi yake aitwaye Felista Masula pamoja na mama mkwe wake na kwamba alidai mbele yao kuwa huyo ni mtoto aliyemzaa bada ya awali kuwahadaa kwambia ni mjamzito.
Kamanda Mtafungwa alisema Jeshi la Polisi baada ya kufanya mahojiano ya kina na mtuhumiwa Martha alikiri kumwiba mtoto huyo ili amwoneshe mume wake na wakwe zake kuwa amepata mtoto kwa madai kuwa alikuwa na hamu ya kupata mtoto siku nyingi na amekuwa akishika ujauzito unaharibika.
“Mtuhumiwa tumemkamata na tutamfikisha mahakamani. Mtoto alipelekwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na kisha amekabidhiwa kwa mama yake,” alisema Kamanda Mtafungwa.