Mtoto aua, ajeruhi wawili kwa risasi

HELSINKI, FINLAND: MTOTO mmoja amefariki na wengine wawili kujeruhiwa vibaya katika shambulizi la risasi katika shule ya Msingi Viertola iliyopo katika jiji la Vantaa nchini Finland.

Polisi nchini humo wamesema mtuhumiwa alikuwa na umri wa miaka 12 na walioshambuliwa pia wana miaka 12 na wote ni wanafunzi wa shule hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la nchini humo, YLE, tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 2 asubuhi, ambapo mshukiwa baada ya kutenda shambulio hilo alikimbia kwa miguu, lakini baadaye alikamatwa na polisi Kaskazini mwa mji mkuu wa Finland Helsinki.

Bunduki iliyotumika katika ufyatuaji risasi ilikuwa na leseni inayomilikiwa na ndugu wa karibu na mtuhumiwa, shirika hilo la utangazaji lilieleza kwamba polisi hawakuwa na maelezo kuhusu nia ya mtoto huyo kutenda shambulio hilo na tayari ameshafunguliwa mashtaka ya mauaji na kujaribu kuua.

Shule ya msingi ya Viertola iko umbali wa kilomita 18 kaskazini mwa Helsinki. Ina karibu wanafunzi 800 kati ya darasa la kwanza na la tisa na ina wafanyakazi karibia 90.

Waziri Mkuu Petteri Orpo amesikitishwa na tukio hilo akisema ni tukio la kushitua
Mnamo mwaka wa 2007, Pekka-Eric Auvinen, mwanafunzi wa sekondari mwenye miaka 18, alifyatua risasi shuleni katika mji wa Tuusula, kusini mwa Finland na kuwaua watu nane, kuwajeruhi wengine 10 kabla ya kujipiga risasi yeye mwenyewe huku akiwa ameacha barua ya kuiaga familia yake.

Mwaka 2008, miezi michache tu baada ya shambulio la Tuusula, Matti Juhani Saari, 22, alifyatua risasi katika shule nyingine nchini humo na kuwaua watu 10 kabla pia ya kujipiga risasi.

Baada ya ufyatuaji risasi, serikali ilitoa miongozo mipya kuhusu matumizi ya silaha hasa bunduki na bastola.

Habari Zifananazo

Back to top button