Mtoto kuiwakilisha nchi mkutano wa usalama

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima

WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imesema Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza mtoto Victor Paschal kwa kuchaguliwa kushiriki katika mkutano wa Baraza la Watoto la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri wa wizara hiyo, Dk Dorothy Gwajima alisema hayo Dar es Salaam na akahimiza watoto wengine wajiunge katika mabaraza hayo ili watambuliwe vipaji vyao na wapewe fursa kuiwakisha Tanzania kimataifa.

Dk Gwajima alisema hayo wakati akimkabidhi bendera ya Taifa, mwanafunzi huyo wa wa darasa la sita anayekwenda kuiwakilisha Tanzania katika mkutano baraza hilo nchini Denmark kuanzia Septemba 13 hadi 16 mwaka huu.

Advertisement

Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoto ili kukabili vitendo vya kikatili  ikiwa ni pamoja na kuimarisha na kuanzisha mabaraza, madawati na majukwaa shuleni kusaidia kujitambua, kujiamini na kufikia ndoto zao.

Dk Gwajima alisema Rais Samia ameruhusu mabaraza hayo mashuleni hivyo ni muhimu wazazi kuwahimiza watoto wajiunge.

“Serikali itaendelea kusimami Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2018 na kutoa maelekezo kwa wadau ilikuhakikisha watoto wanashirkishwa katika masuala yanayowahusu kama ambavyo sheria ya mtoto ya mwaka 2019 inasisitiza ushirikishwaji wa mtoto katika masuala yanayowahusu,”alisema.

Dk Gwajima alisema pia serikali inaendelea kutekeleza mkataba wa kimataifa wa mwaka 1989 unaoelekeza nchi mwanachama kuruhusu mtoto kuwasilisha mawazo yake, kusikilizwa kwa uhuru kulingana na umri wake.

Alisema mabara ya watoto shuleni yanawasaidia kuwajengea uwezo wa uongozi, uzalendo, maadili mema, kutambua na kuepuka maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi, Teknolojia ya habari na mawasiliano (tehama).

“Pia wanafundishwa masuala ya jinsia na kudhibiti ukatili inapotokea na kuepuka mimba za utotoni, Pia yanawasaidia kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuimarisha uhusiano miongoni mwa watoto hivyo nivyema wataendeleza na kuimarisha,”alisema Dk Gwajima.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo na Watoto iliyoko chini ya Wizara hiyo, Sebastian Kitiku alimpongeza mtoto Victor kuwa miongoni mwa watoto saba waliochaguliwa katika bara la Afrika ambaye ataungana na watoto 80 kutoka duniani kote watakaoshiriki katika mkutano huo wa usalama.

“Hii ni mara ya pili kwa watoto wetu kuchaguliwa kushiriki katika mkutano huo wa kimataifa ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2014 alipochaguliwa Getruda kuiwakilisha Tanzania katika mkutano huo wa watoto,” alisema Kitiku.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Pascal Tantau alipongeza serikali kwa kumsaidia na kumkabidhi Victor bendera ya nchi kushiriki katika mkutano huo.

Victor alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua juhudi zake hivyo ataiwakilisha vyema Tanzania ili kuleta hamasa zaidi kwa watoto wengine.