Mtoto wa Rais wa zamani kukamatwa kwa ufisadi

MWANASHERIA Mkuu wa Angola Helder Pitta Groz amethibitisha kuwa nchi yake imetoa hati ya kukamatwa kwa binti wa  Rais wa zamani wan chi hiyo Jose Eduardo dos Santos, Isabel dos Santos.

Kwa mujibu wa  tovuti ya Angop imemnukuu Groz akisema kuwa  mamlaka ya Angola imekua  inataka kukamatwa kwa Bi dos Santos, Mkuu wa zamani wa kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, kupitia Interpol, baada ya kushindwa kumpata na hakuna majibu kutoka kwake au mawakili wake licha ya kupelekewa maombi ya kuitwa mara kadhaa kwa mahojiano.

Interpol hutoa ” hati nyekundu’ ambayo ni maombi kwa mashirika ya kutekeleza sheria ulimwenguni kote kutafuta na kumweka kizuizini mtu.

Hata hivyo hadi  kufikia leo  Jumanne asubuhi, hakuna taarifa kama hiyo  ya Bi dos Santos iliyoorodheshwa katika kanzi data ya  mtandaoni wa Interpol.

Kwa mujibu wa Groz, amedai kuwa serikali ya Angola imekuwa ikifanya kazi na Interpol kumtafuta Bi Dos Santos ambaye ameshtakiwa na mamlaka ya nchi hiyo  kwa matumizi mabaya na ubadhirifu wa fedha za umma alipokuwa akiongoza kampuni ya mafuta ya serikali, Sonangol.

Taarifa zinasema dos Santos (49) anatafutwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya utakatishaji fedha, utapeli na kutumia vibaya mamlaka.

Anakabiliwa pia na tuhuma za rushwa kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na madai ya Angola ya mwaka 2020 kwamba yeye na mumewe walikuwa wametoa dola bilioni 1 katika fedha za serikali kwa makampuni ambayo walikuwa na hisa wakati wa urais wa baba yake, ikiwa ni pamoja na kampuni kubwa ya mafuta ya Sonangol. Isabel dos Santos mara kwa mara amekana kuhusika na makosa hayo.

Katika mahojiano na The New York Times alisema kwamba alikuwa tayari kuhojiwa. “Anwani yangu inajulikana, nilipo panajulikana,” aliambia gazeti hilo.

“Mimi si mkimbizi. Sijifichi kwa  mtu yeyote, “aliongeza, akisema kwamba alikuwa akiishi London. Pia alielezea shutuma hizo kuwa ni za kisiasa.

Babake Isabel dos Santos, Jose Eduardo dos Santos, alifariki dunia Julai mwaka huu baada ya kutawala Angola kwa takriban miongo minne hadi 2017.

Wakati mmoja Isabel dos Santos aliwahi kutajwa kuwa mwanamke tajiri zaidi barani Afrika huku utajiri wake ukikadiriwa kuwa dola bilioni 3.5.

 

Habari Zifananazo

Back to top button