Mtoto wa Simbachawene ahukumiwa faini au jela miezi 18

MAHAKAMA ya Wilaya Kinondoni mkoani Dar es Salaam imemtia hatiani na kumhukumu, James Simbachawene (24) alipe faini ya shilingi 250,000 au kifungo cha mwaka mmoja na miezi sita gerezani.

Mahakama hiyo pia imeifungia leseni ya udereva ya kijana huyo kwa miezi sita.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Aron Liyamuya alisoma hukumu hiyo jumatano. Akisoma hati ya mashitaka wakili wa serikali, Daisy Makakala alidai kuwa Agosti 20 mwaka huu katika barabara ya Haile Selasie eneo la Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro wilayani Kinondoni mshitakiwa aliendesha gari aina ya Toyota Crown lenye namba za usajili T 670 DKG na aligonga gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili 344 DKG.

Makakala alidai kuwa baada ya kugonga gari hilo mshitakiwa alijaribu kutoroka na aligonga kwa nyuma gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 370 DWY lililokuwa limesimama kwenye taa za kuongozea magari.

Katika shitaka la pili alidaiwa kuwa katika tarehe na sehemu tajwa mshitakiwa aliendesha gari akiwa amelewa na kwamba baada ya kukamatwa mshitakiwa alipimwa na kukutwa na kiwango cha pombe 184.3mg/100ml.

Katika shitaka la tatu ilidaiwa kuwa katika tarehe na sehemu tajwa mshitakiwa alikamatwa akiendesha gari aina ya Toyota Crown lenye namba T 760 DKG bila kuwa na bima.

Daisy alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuna vielelezo vitatu ambavyo ni ramani ya mchoro eneo la tukio, ripoti ya uharibifu wa magari na ripoti ya kipimo cha pombe na aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Mshitakiwa akiongozwa na wakili wake, Alfred Mtawa alikiri makosa yote na aliiomba mahakama imsamehe kwa kuwa ana mtoto mdogo, mke na ni mara ya kwanza kutiwa hatiani

Habari Zifananazo

Back to top button