Mtuhumiwa wizi kwenye ajali ajinyonga
MTUHUMIWA Said Kibula (69), aliyepandishwa kizimbani kwa tuhuma za wizi wa mizigo ya marehemu na majeruhi wa ajali iliyoua watu 20 hivi karibuni Mombo, wilayani Korogwe mkoani Tanga, amekutwa amejinyonga shambani kwake kwa kutumia chandarua.
Kibula ni kati ya watuhumiwa 8 wa tukio la wizi wa mali mbalimbali katika ajali iliyotokea hivi karibuni wilayani Korogwe mkoani Tanga ikihusisha gari aina ya Fuso iliyogongana na Coaster, iliyobeba mwili wa marehemu pamoja na waombolezaji wakitokea Dar es salaam kuelekea Moshi, Kilimanjaro kwa mazishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Chidindi amesema mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Magira Gereza alikuwa nje kwa dhamana ya mahakama ya Hakimu Mkazi Korogwe, ambapo alikutwa amejinyonga usiku wa kuamkia Februari 23, 2023.
Akizungumza jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba alisema waliwakamata watuhumiwa 12 kuhusu wizi katika gari hiyo ya ajali na kwamba 8 ndiyo walifikishwa mahakamani mwanzoni mwa wiki hii, akiwemo Kibula ambaye anatuhumiwa kukutwa na nguo za marehemu wa ajali zikiwa na damu.