KATAVI; Mpanda Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi, Jamila Yusuf amempa siku saba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kuhakikisha aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kamakuka Kata ya Kakese, anarudisha kiasi cha Sh 250,000 alichokusanya michango ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Kijiji akidaiwa kukimbia nazo.
Akiwa katika ziara ya kusikiliza kero za wananchi kijijini hapo, DC Jamila amesema licha ya ofisa huyo kutakiwa kuzirudisha fedha hizo anatakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
Hoja hiyo iliibuliwa na wananchi baada ya kushindwa kuendelea na ujenzi huo kwa kile wanachodai michango yao inaliwa na viongozi.
Akizungumzia tukio hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Deodatus Kangu amesema taarifa hiyo ipo ofisini kwake muda mrefu na tayari mpango ni kukata kwenye moja ya malipo anayodai mtendaji huyo, kitendo ambacho Mkuu wa Wilaya amekataa na kuagiza mtendaji huyo akatwe kwenye mshara wake, ili fedha hiyo irudi kwa wananchi.