Mtusate sasa ina bil 51.99/- za uendelezaji sayansi

SERIKALI imefanikiwa kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) ambao mpaka sasa umepokea zaidi ya Sh bilioni 51.99.

Naibu Katibu Mkuu, Prof Carolyne Nombo alisema hayo Alhamis alipomwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda wakati wa kufungua warsha ya siku mbili ya kupitia na kujadili Rasimu ya Sera ya Taifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu nchini.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, imeendelea kuwekeza katika kujenga uwezo na mazingira rafiki nchini ili kuongeza kasi ya maendeleo na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukuza uchumi, kuongeza pato la Taifa na kuboresha maisha ya Watanzania kwa ujumla.

Advertisement

Aidha, Profesa Nombo alisema katika utekelezaji wa Sera ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1985, 1996 na mikakati mingine ya kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu vimesaidia kuimarisha maendeleo na matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii nchini.

Alisema mafanikio mengine yaliyofikiwa wakati wa kutekeleza sera hiyo ni kuongezeka kwa taasisi za utafiti na maendeleo nchini kutoka 18 mwaka 1961 hadi kufikia taasisi 94 mwaka 2021.

Alisema pia kupandisha hadhi kwa Chuo cha Ufundi cha Dar es Salaam na kuwa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (1997) na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya (2006) kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (2012).

“Kutokana na mabadiliko hayo vyuo hivi vimeongeza uwezo katika shughuli za kitaaluma na utafiti katika sayansi na teknolojia huku mwaka 2011, Serikali ilianzisha rasmi Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwa kitovu utafiti, ugunduzi na ubunifu wenye hadhi ya kimataifa.”

Alisema pia kuongezeka kwa Taasisi za Elimu ya Juu ambazo pia zinajihusisha na utafiti na ubunifu kutoka Chuo Kikuu kishiriki kimoja hadi kufikia Vyuo Vikuu 47 mwaka 2021 na kuongezeka kwa vituo vya bunifu na Atamizi hadi kufikia vituo zaidi ya 45 kufikia mwaka 2022.

Alisema pia kumekuwapo na ongezeko la idadi ya watafiti kutoka taasisi za elimu ya juu na taasisi za utafiti na maendeleo za umma kutoka 3,593 mwaka 2007/08 hadi 10,966 mwaka 2021.

Pia kuzalisha teknolojia mbalimbali zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, uzalishaji wa mbegu mpya za mazao na wanyama, chanjo mpya za magonjwa ya mifugo, teknolojia rahisi za kusafisha maji ya kunywa (nanofilter), mtambo mdogo wa kuzalisha sukari n.k.

Alisema pia uanzishwaji mifumo mbalimbali ya kuibua, kutambua na kuendeleza wabunifu na bunifu zinazozalishwa katika ngazi mbalimbali nchini ikiwemo mfumo usio rasmi.

Alisema pia kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika Global Innovation Index inayopima uwezo wa nchi katika kufanya ubunifu wenye tija katika uchumi.

“Tanzania ni moja kati ya nchi tano Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa miongoni mwa nchi 100 duniani zinazofanya vizuri katika masuala ya ubunifu wenye tija.”

Alisema pamoja na mafanikio hayo, Serikali imeona haja ya kupitia sera hiyo ili kuakisi mahitaji na kasi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kitaifa na kidunia.

Awali, Mkurugenzi, Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Maulilio Kipanyula alisema mchakato wa kupitia na kuhuisha sera hii ulianza miaka kadhaa iliyopita ikihusisha kupata maoni ya wadau mbalimbali kutoka katika sekta za umma na binafsi.

Alisema mbali na sera pia kuna kupitia rasimu ya Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu ambacho kimelenga kuimarisha uratibu na usimamizi wa masuala ya ubunifu katika ngazi mbalimbali nchini.

“Kupitia Kiunzi hiki tutaweza kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wadau mbalimbali kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu wenye tija nchini.”

Naye Mwakilishi Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, Unesco, Faith Shayo alisema ni imani ya Unesco kuwa mapitio ya nyaraka hizo yatazingatia maazimio ya nchi wanachama wa Unesco kuhusu utafiti na watafiti wa kisayansi ya mwaka 2017.

Alisema pia matarajio ya mapitio ya nyaraka hizo zitahamasisha bunifu za ndani katika ngazi za chini na kuweka utaratibu wa kuzitambua na kuzikubali, kuziendeleza, kuzirasimisha na kizibisharisha.

“Pia kupunguza matumizi ya Teknolojia zisizoakisi mazingira halisi ya Watanzania walio wengi ambao ndio wahitaji na watumiaji wa bunifu mbalimbali.”

Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Jerry Silaa alisema katika eneo litakalotoa tija ya kupunguza tatizo la ajira nchini ni ubunifu.

“Wako vijana wengi wamejiajiri katika maeneo mbalimbali lakini bunifu za ndani zinaweza kuwa na suluhisho la changamoto za ndani, hivyo mapitio haya ni muhimu sana.”

Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Aloyce Kamamba alisisitiza haja ya maboresho ya nyaraka hizo ili kuweza kusaidia vijana wa Tanzania kupitia bunifu na ubunifu wao.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *