MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA), imesaini mikataba miwili na wakandarasi kwa ajili ya kujenga miradi ya kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika Halmashauri ya Mji Nanyamba na Halmsahauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Mikataba hiyo imesainiwa leo Julai 6,2023 kati ya MTUWASA na wakandarasi hao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo, Mkurungezi Mtendaji wa MTUWASA, Mhandisi Rejea Ng’ondya amesema moja ya miradi hiyo unalenga kuboresha upatikanaji wa maji kwenye hospital ya Rufaa Kanda ya Kusini iliyopo Mitengo, Mtwara.
Mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni moja na utajengwa moja kwa moja kuhudumia hospitali peke yake.
Ng’ondya amesema ujenzi wa mradi huo utahusisha ununuzi wa mabomba na kujenga matenki ya maji.
“Mradi mwingine umelenga kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji kwenye maeneo ya Halmashauri ya Mji Nanyamba hasa mradi wa Mnyawi ,” amesema.
Ng’ondya amesema mradi huo utagharimu kiasi cha Sh bilioni 5.6 na utahusisha ujenzi na uboreshaji wa chanzo chenyewe na mabomba.
Akizungumzia hatua hiyo mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa ukarabati wa mradi huo utaenda kuondoa kero kubwa kwa wakazi wa mji huo kwani kumekuwa na kilio cha muda mrefu kwa wakazi hao.
“Nichukue fursa hii kumpongeza rais wetu daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kumtua ndoo mama kichwani sie wakazi wa jimbo la Nanyamba hatuna cha kumlipa zaidi ya kumuombea kwa mwenyezi Mungu kwa kuweza kutushika mkono.” amesema Chikota
Comments are closed.