Mtwara wazindua kampeni chanjo ya rubella

KAIMU Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, John Nkoko amezindua kampeni ya chanjo ya surua rubella kwa watoto wenye umri kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano.

Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 16, 2024 katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Nanguruwe mkoani Mtwara.

Akizungumza katika ufunguzi huo, Nkoko amesema halmashauri hiyo imelenga kutoa chanjo kwa watoto 17,513, hivyo amewataka wazazi na walezi kuwalinda watoto hao kwa kuwapeleka kupata chanjo ili waweze kukua na kutimiza malengo yao.

“Ugonjwa huu wa surua una madhara makubwa sana kama alivyozungumza daktari kila mtu angependa kumuona mtoto wake anapozaliwa anakua na zile ndoto ambazo umemuombea akishakua mtu mzima azifikie”

“Hamna mtu ambae anapenda kumuona mtoto wake anakuwa baada ya muda mfupi anapata maradhi ya kudumu, ili kuwakinga watoto wetu waweze kuwa madaktari, wakurugenzi.”amesema Nkoko

Amewaomba wazazi,walezi waliofika kwenye ufunguzi huo kuwa mabalozi kwa wananchi wenzao ili kuhakikisha watoto wote wanapatiwa chanjo hiyo.

Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Joel Tiho amesema chanjo hiyo haina madhara yoyote na ni kinga dhidi ya ugonjwa wa surua kwa watoto hao.

Hata hivyo dalili kubwa ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kutoka vipele vidogo vidogo, mafua, kutoka usaha au uchafu masikioni na kupata shida ya macho.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nanguruwe kwenye halmshauri hiyo, Ahmed Chikalengele amesema tayari wameanza kutoa hamasa kwa wazazi na walezi ili waweze kupeleka watoto wakapate chanjo itakayo wafanya kujiepusha na matatizo yanayoweza kuzuilika.

Chanjo ya surua rubella imeanza kutolewa Februari 15 na kukamilika Februari 18, 2024 yenye kauli mbiu inayosema “Mpende Mwanao Mpeleke Akapate Chanjo”

Habari Zifananazo

Back to top button