Mtwara waanza maandalizi uzinduzi wa Mwenge
MKOA wa Mtwara unatarajia kufanya mkutano wa watoa huduma za kijamii wakiwemo wafanyabiashara, ili waweze kutoa maelekezo namna watakavyoshiriki katika uzinduzi wa Mwenge kitaifa Aprili 2 mwaka huu mkoani Mtwara.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema hayo leo wakati akitoa taarifa kuhusu ratiba za matukio mbalimbali ya maandalizi ya uzinduzi wa mwenge huo 2023.
Amesema mkutano huo utatanguliwa na matukio mengine ikiwemo tukio la matembezi ya hisani mkoani humo, ambalo litafanyika Machi 18 mwaka huu.
“Tukio hilo kinatarajiwa kuhudhuriwa na washirika zaidi ya 5,000 wakiwemo viongozi mbalimbali,” amesema.
Ametaja matukio mengine kuwa ni makongamano makubwa ya wanawake katika maeneo mbalimbali mkoani Mtwara yatakayoambatana na maenesho ya shughuli za mwanamke zitakazobeba ujumbe wa mwenge.
“Ndani ya mwezi Machi pia tunatarajia kuwa na Juma la Elimu ambalo pia kutakuwa na mlolongo wa matukio ikiwemo semina, mashindano ya uandishi wa insha na midahalo,” amesema.
Matukio mengine ni utekelezaji wa shughuli za kijamii, ambapo kila halmshauri Kwa kushirikiana na wananchi watakuwa na ratiba za shughuli za maendeleo watakazozitekeleza.
Mkoa huo pia utakuwa na wiki ya maonesho ya bidhaa na shughuli mbalimbali katika viwanja vya Mashujaa ,ambapo taasisi mbalimbali zitapewa fursa ya kuonesha bidaa zao na pia kujitangaza.
Zaidi ya wageni 1000 wanatarajia kuhudhuria uzinduzi wa mwenge 2023 kitaifa Aprili 2 katika viwanja vya Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.