MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Dustan Kyobya, amewataka wakuu wa shule za msingi na sekondari wilayani humu kuweka mikakati ambayo itawezesha wanafunzi kupata chakula wakiwa shuleni.
Amewataka wakuu hao kutengeneza bustani kwa ajili ya mazao ya chakula cha wanafunzi shuleni na endapo shule zao zina eneo kubwa waanze kulima mazao ya chakula na biashara kwa ajili ya kujipatia kipato cha shule.
“Kwanza kila shule lazima ihakikishe inakuwa na hati ya eneo la shule, mkatengeneze bustani kwa ajili ya mazao ya chakula, kama kuna eneo kubwa mlime mazao ya chukula na biashara kwa ajili ya kipato cha shule,” amesema.
Alitoa maagizo hayo wakati akikabidhi vitabu vitatu vya kimkakati vya kutoa miongozo na mikakati ya kuboresha elimu msingi na sekondari, pamoja na kuimarisha uongozi katika ngazi za shule, kata, halmashauri pamoja na mikoan kwa maofisa elimu na walimu wakuu wilayani humu.
Vitabu hivyo vilizinduliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Agosti 4, mwaka huu katika ufunguzi wa mashindano ya Michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) pamoja na mashindano ya Michezo ya shule za sekondari (UMISSETA) mkoani Tabora, na baadae kuzinduliwa kwa mikoa na wakuu wa mikoa nchini.