Mtwara watoa msaada waathirika Hanang

SERIKALI ya Mkoa wa Mtwara imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara wenye thamani ya takribani Sh milioni 25.

Akizungumza leo mkoani Mtwara wakati akikabidhi vifaa hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas amesema mkoa huo kwa kushirikiani na wadau mbalimbali ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza agizo la serikali la kuzilekeza mamlaka za mikoa kuhakikisha zinashirikiana na wadau mbalimbali kupata misaada ya hali na mali itakayowezesha kwenda kuwashika mkono waliyopatwa na majanga hayo.

Mafuriko hayo yalitokea kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Disemba 3, 2023 na kusababisha maporomoko ya udongo, magogo na maji kwa wingi kuelekea kwenye makazi ya watu, maeneo ya shughuli za kiuchumi na kijamii lakini pia uharibifu wa miundombinu, majeraha kwa watu na vifo kwa baadhi ya wananchi.

Advertisement

Msaada huo umetolewa leo Disemba 27, 2023 ikiwa ni pamoja na magodoro 100, saruji mifuko 625, ndoo 100, mifuko ya chumvi kilogram 250, nguo, unga wa sembe mifuko 125 pamoja na vingine ambapo mkoa unahamasisha wananchi kutoa michango ili kuendelea kuwashika mkono waathirika hao.

‘’Pamoja na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kuu lakini sisi kama mkoa wa Mtwara tumeguswa na maafa yale na tunaendelea kutoa pole nyingi kwa wote waliyoathirika kwenye tukio hilo na ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza agizo hilo la serikali ’’amesema Abbas.

“Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inawaomba wananchi wa mtwara kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwa wananchi wezetu wa wilaya ya Hanang ili kuwatia moyo na niendelee kuwashukuru wote ambao wameshatoa misaada hiyo niliyoisema na kuendelea kuwasisitiza wengine kuendelea kutoa’’

Aidha, serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na ofisi za wakuu wa mikoa inaendelea kuratibu hatua za kuweza kukabiliana na maafa hayo na kuzilekeza mamlaka za mikoa kuhakikisha zinashirikiana na wadau mbalimbali kupata misaada ya hali na mali itakayowezesha kwenda kuwashika mkono waliyopatwa na majanga hayo.