Mtwara yajidhatiti kutangaza utalii

SERIKALI ya Mkoa wa Mtwara imeendelea kutangaza utalii na uwekezaji kwa kuonesha vitu mbalimbali vya kitalii vilivyopo ndani ya mkoa huo.

Akizungumza jana katika tamasha la mkesha wa kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya 2024 iliyofanyika katika kata ya Msangamkuu Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani humo (Msangamkuu Beach Festival) msimu wa nne, Mkuu wa  Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema lengo la tamasha hilo ni kutangaza utalii na uwekezaji ndani ya mkoa huo.

‘’ Msangamkuu Beach Festival ni mwendelezo wa sizoni moja, mbili mpaka tatu na makusudio ya hii kitu ni kutangaza utalii na uwekezaji ndani ya mkoa wa mtwara, mambo haya tunayafanya kwa kuonyesha vitu mbalimbali vya kitalii lakini vile vile kuwaambia wanaokuja hapa kushiriki fursa gani zipo ndani ya mkoa wa mtwara’’amesema Abbas

Aidha wadau mbalimbali wameshiriki katika tamasha hilo ikiwemo mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini (TPA) mkoa wa Mtwara, Tra, taasisi za kifedha na wengine huku wakipatiwa taratibu wanazotakiwa kuzifata kama vile za kikodi, kiusalama pamoja na za kibiashara.

‘’Kwetu sisi hili tunaloliona ni tamasha kubwa lakini ukiacha makusudio haya tunayoyasema pia ni sehemu ya kuwakutanisha wananchi wa mkoa wa mtwara na wangeni waliyokuja kutembelea kwenye mkoa wetu hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na sikukuu za mwisho wa mwaka ili wapate sehemu salama wanayoweza kupata burudani’’

Aidha licha ya wananchi mkoani humo kujitokeza kushiriki tamasha hilo lakini amewaomba na kuwasisitiza kuendelea kushirikiana na uongozi wa mkoa huo katika mambo ikiwemo  hayo ya tamasha na wakati wanashiriki wahakikishe wanashiriki kwa amani, utulivu na upendo mkubwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amesema matarajio na malengo ya mkoa huo ni kuwa na tamasha kubwa litalowakutanisha wanamtwara wote mkoa mzima ili kueleza na kuonyesha tamaduni mbalimbali zilizopo ndani ya mkoa ikiwemo ngoma za asili na uwepo wa wasanii wengi wanaotoka ukanda huo wa Kusini.

 

Habari Zifananazo

Back to top button