Mufindi Kusini waomba mbolea ya ruzuku

MADIWANI, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa matawi na kata Jimbo la Mufindi Kusini wameiomba serikali kuwapelekea mbolea ya ruzuku ambayo imeadimika vijijini.

Viongozi wameyasema hayo kwa nyakati tofauti Januari 2, 2023 katika kikao  cha tathmini ya utendaji mwaka 2022 na kuweka mkakati  wa pamoja wa kujipanga kwa maandalizi ya uchaguzi wa  serikali za mitaa 2024.

Kikao hicho kiliitishwa na Mbunge wa Mufindi Kusini,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge la Tanzania, David Kihenzile.

Wakizungumza kwenye mkutano huo maalumu wa ndani, viongozi hao wameishukuru serikali ya CCM inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuweka ruzuku kwenye mbolea, ambapo mwaka huu inauzwa Sh  70,000 kwa mfuko baadala ya Sh  130,000 iliyokuwepo mwaka 2021

Akifungua Kikao hicho, kilichofanyika ukumbi wa Masangula, Igowole Mwenyekiti wa CCM Wilaya Mufindi, George Kavenuke, alisema uhaba wa mbolea ya ruzuku imekua changamoto kubwa inayopigiwa kelele na wananchi wa Mufindi na kuiomba serikali isikie kilio hicho na kupeleka mbolea, huku akimwagia sifa Mbunge wa Jimbo hilo David Kihenzile kwa utendaji mzuri.

“Mufindi Kusini mmepata kiongozi, mshikilieni, mbadala wa Mungai (Joseph) amepatikana, anafanya makubwa katika sekta ya barabarani, Mungai enzi zake alituita wote kama hivi na  chinja ng’ombe, tulikula na kufurahi, Kihenzile  naye hivyo hivyo, huu ndio uongozi, kukaa na watu kula pamoja,” alisema.

Naye  Mbunge Kihenzile akizungumza na HabariLEO kwa njia ya simu, wakati  akihitimisha hoja na majumuisho ya mikutano hiyo aliiomba serikali iingilie kati jambo hilo mara moja, ili dhamira ya serikali kushusha bei iweze kunufaisha wananchi wa Mufindi na Watanzania kwa ujumla.

“Mbolea kwetu haipatikani ndio changamoto kubwa, naomba serikali isaidie kupatikana, tuna changamoto kubwa sana, imekua ni kero zaidi licha ya kwamba serikali ilitoa ruzuku, lakini mbolea haipatikani, ” amesema Kihenzile.

Kihenzile amesema katika mkutano huo, viongozi hao pamoja na kukubaliana kila tawi kukamilisha mpango kazi na vipaumbele vya tawi na kata,  pia wameiomba CCM vitendea kazi mbali mbali.

Amesema viongozi hao pia wameishukuru serikali ya CCM kwa ujenzi wa barabara ya Sawala Luhunga km 30 sambamba na kukubali kumalizia kipande kilichobaki cha Kilometa 10 kwenda Iyegea.

” Lakini zaidi wamefurahishwa sana serikali yao kwa mara ya kwanza kupitisha bajeti ya ujenzi wa  kiwango cha lami cha  barabara za Mafinga-Mgololo Kilometa 78 na Nyololo-Mtwango Kilometa 40.4,”amesema Kihenzile na kuongeza:

“Viongozi hao wa CCM wamefurahishwa sana na Mpango wa serikali kuanza Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA, sambamba na kuanza ujenzi wa kiwanda cha parachichi Kata ya Nyololo.”

Habari Zifananazo

Back to top button