MUHAS kuwashika mkono wabunifu

DAR ES SALAAM: CHUO cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimekusanya Sh milioni 10 kwa ajili ya kuhamasisha watumishi na wanafunzi kusajili bunifu zao na kuwasaidia kupata wadau kuendeleza bunifu zao.

Fedha hizo zimetokana na matembezi ya hisani ya kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.

Akizungumza baada ya matembezi hayo leo Dar es Salaam, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema walikuwa na matembezi ya Kilometa 1, 5,10 na 15 na lengo ni kuendeleza tafiti na bunifu zinazofanywa na wanafunzi chuoni kupitia Kitengo cha Bunifu na Tafiti.

Amesema kuwa matembezi hayo yamehusisha wanafunzi mbalimbali waliosoma chuoni hapo miaka iliyopita, familia zao na marafiki zao.

“Haya ni matembezi ya pili tulianza mwaka 2022 na huu ni muendelezo na muitikio unazidi kuwa mkubwa hivyo, tuendelee kuhamasisha wadau kuunga juhudi hizi,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Ameeleza kuwa fedha hizo zitaweza kuimarisha kitengo hicho kwani wamekuwa na vijana wenye ubunifu na wanalenga kutunza vipaji vyao.

Profesa Kamuhabwa amesema bunifu zinazofanywa na vijana hao ni zile zinalenga kusaidia mifumo ya afya kwenye kuchunguza magonjwa, kutibu na matumizi ya akili bandia.

Amesema tafiti za afya ni gharama kwani zinahitaji vifaa, fedha na vitendanishi hivyo wanaendelea kuhamasisha wadau kuona umuhimu wa tafiti katika kuboresha maisha ya watanzania.

Ameongeza kuwa kwa mwaka huu pekee wana miradi 136 yenye ufadhili kutoka mashirika na taasisi mbalimbali hivyo, zimeboresha taswira ya chuo, kutoa majawabu na kuboresha afya za watanzania.

“Mbio hizi zinalenga kuhamasisha kuacha tabia bwete na tunaendelea kuhamasisha watu kufanya mazoezi na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ya kuambukiza ikiwemo moyo, kisukari na shinikizo la damu ambayo husababishwa na mtindo wa maisha,” amesema.

Kwa upande wake, Marsha Macatta yambi – Rais wa Alumnae MUHAS amesema chuo hicho kimekuwa kinawapa hamasa kwani wamekuwa wakisoma na kufanya shughuli mbalimbali hivyo wanarudisha fadhila ili kukamilisha adhma yao ya kusaidia tafiti ambazo zinafanywa na wale wanaoendeleza masomo.

“Katika mbio hizi tumechanga zaidi ya Sh milioni 10 ambazo zitaanzisha vuguvugu za kuendeleza tafiti na kufanya chuo kuwa bora zaidi Tanzania na Afrika,” amesema.

Amesema kwamba dunia ya sasa inahitaji kutafuta suluhisho za matatizo mbalimbali yaliyopo kwenye jamii, hivyo wanafunzi wanapaswa wawe wabunifu ili kuleta mabadiliko chanya.

Ameeleza kuwa kwa kupitia tafiti watapunguza changamoto ambazo zimekuwa kero ikiwemo vifo vya wajawazito na watoto, magonjwa yasiyoambukiza na yakuambukiza hivyo, itasaidia kupiga hatua na kufikia malengo ya maendeleo endelevu yanayohusu afya.

“Wale walio chuo na wanaotaka kuja chuo wanatakiwa kupeana motisha kwa sababu wanahitaji wanawake wengi zaidi wenye utaalamu wa afya,” amesisisitiza.

Habari Zifananazo

Back to top button