MUHAS yajivunia ushirikiano na Sweden
WATAFITI 95 ngazi ya uzamivu kutoka MUHAS wamefaidika katika tafiti na mafunzo kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA).
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden Makamu Mkuu wa Chuo, MUHAS Profesa Aporinary Kamuhabwa amesema, walianzisha ushirikiano huo kwa lengo la kusaidia tafiti na mafunzo kama vile VVU/UKIMWI, kifua kikuu na malaria na kuongeza kuwa zilichangia kutoweka kwa sera ya nchi.
“Sisi kama Chuo Kikuu cha Afya tafiti zetu na mafunzo yetu ziko kwa upande wa Afya na Sayansi Shirikishi, watafiti hawa wamesoma kwa njia za kufanya tafiti hivyo kupitia Sida tumefanya tafiti nyingi zikiwemo za magonjwa ya kuambukiza ambapo mwanzoni tulianza na ukimwi, kifua kikuu na malaria na magonjwa mengine”.
Amesema siku hizi magonjwa yanazidi kubadilika, na kuna magonjwa yasiyo ya kuambukiza hivyo mpango unaoendelea sasa ni kufanya tafiti katika magonjwa yasiyoambukiza na kuja na matokeo chanya.
“Chuo cha MUHAS ni Chuo cha tatu kwa ukubwa katika nchi ziliopo chini ya Jangwa la Sahara, hivyo mnaweza mkaona ushirikiano kama huu unafanya chuo kuweza kutambulika Kimataifa lakini tafiti ambazo zimefanyika kwa kushirikiana na MUHAS zimeweza kutoa majibu yanayolenga kutatua matatizo na changamoto za wananchi” amesema Kamuhabwa
Profesa Kamuhabwa ameongeza kuwa, ushirikiano huo pia umeiwezesha MUHAS kupata, teknolojia mpya zaidi huku tafiti zake zimechangia sana mabadiliko ya dawa haswa zile za malaria.
Wakati wa Covid-19, MUHAS ilifanya utafiti juu ya chanjo, dawa na kinga
Ameongeza kuwa, mpango ulikuwepo wa mashirikiano kati ya SIDA na MUHAS wa 2015 unaenda kufikia ukingoni na wanatarajia kuingia makubaliano mapya ambayo yanatarijiwa kusainiwa Novemba mwaka huu.
Amesema mpango huo utakaodumu hadi mpaka 2026 utakuwa ni muendelezo wa kuendelea kutoa mafunzo kwa wanataaluma na kufanya tafiti.
Kwa upande wa Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Marcias amesema SIDA imekuwa ikitoa fedha za maendeleo katika mioundombinu ya Tehama, tafiti na mafunzo.
Aidha, amezindua maabara ya Biorepository na kituo cha ubunifu maeneo yote katika chuo cha MUHAS Mloganzila.