MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa mazingira Tanga, imeingia mkataba wa Sh Bil 3.1 na Kampuni inayosimamia ujenzi wa Bomba la mafuta (EACOP), kwa ajili ya uboreshwaji wa huduma ya maji kwenye Wilaya za Muheza na Tanga.
Akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini mkataba huo, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amesema mkataba huo utasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, kwenye maeneo ambayo yalikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.
“Hii ndio tunaita kurudisha kwa jamii, kwani wananchi wengi wanakwenda kunufaika na mradi wa bomba, lakini na kupata fursa ya huduma ya maji safi na salama,”amesema Waziri Ummy.
Naye Mkurugenzi wa Tanga UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly amesema kuwa fedha hizo zitatekeleza miradi miwili ya maji, huku zaidi ya wananchi 30,000 watanufaika na huduma hiyo.
Msimamizi wa ujenzi kituo cha Tanga kutoka shirika la EACOP, Jerome Betat, amesema mradi huo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii iliyopo karibu na maeneo ya mradi.