DAR ES SALAAM; HOSPITALI ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa Macho kutoka Korea inatarajia kuweka kambi maalumu ya upasuaji wa macho kwa njia ya matundu madogo kwa siku saba.
Upasuaji huo utaanza kufanyika Novemba 27 hadi Disemba 2, 2023 kwa kushirikiana na Taasisi ya Vision Care.
Mkuu wa Idara ya Macho MNH Upanga, Dk Joachim Kilemile amesema upasuaji huu ni tofauti na uliokuwa unatumika awali ambapo mgonjwa alikuwa anapasuliwa sehemu kubwa ili kuweza kutoa mtoto wa jicho.
“Upasuaji huu ni wa kisasa zaidi mgonjwa atapasuliwa sehemu ndogo tofauti na ilivyokuwa ikifanyika awali na kwamba katika Hospitali za Umma Muhimbili ni hospitali pekee ambayo inatoa huduma hii.”amesema Dk. Kilemile
Akizungumzia faida za upasuaji huu Dk. Kilemile amesema una faida nyingi kwakuwa mgonjwa atapona kwa muda mfupi na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.
“Mgonjwa atahudumiwa na kuruhusiwa siku hiyo hiyo kurejea nyumbani, atapona kwa muda mfupi na kuweza kuendelea na ratiba zake za kila siku ambapo awali mgonjwa alikuwa akifanyiwa upasuaji inamchukua zaidi ya wiki moja kupona na kurudi katika hali yake.” Amefafanua Dk. Kilemile
Hivyo Dk. Kilemile ametoa wito kwa wagonjwa wote wenye changamoto ya mtoto wa jicho kufika Muhimbili Upanga kwa ajili ya kupata matibabu hayo. Kwa maelezo zaidi na kuweka miadi (appointment) unaweza kuwasiliana kupitia namba za simu: 0713-209056/ 0758 261 493 / 0713 091 664.
Comments are closed.