Muhimbili yatumia saa 6 kutenganisha mapacha

Mifuko ya Plastiki marufuku Muhimbili

DAR ES SALAAM: SAA sita zimetumika kuwatenganisha watoto mapacha wa kike wenye umri wa miezi 10 wakazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Watoto hao ambao walizaliwa Machi mwaka jana walikuwa wameungana eneo la kifua na tumbo. Upasuaji huo ni wa kwanza kufanywa na madaktari wazawa hapa nchini.

Akizungumza leo Januari 30, 2024, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Dk Rachel Mhaville amesema upasuaji huo umefanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa tiba vya kisasa pamoja na kuwasomesha wataalamu.

Advertisement

“Tunachojivunia katika upasuaji huu ni kuwa umefanywa na timu ya madaktari wazawa, umefanyika kwa mafaniko makubwa na watoto wanaendelea vizuri kabisa.

Amesema, hata hivyo pamoja na kufanikiwa kufanya upasuaji huu bado tutaendelea kushirikiana na wataalamu wengine kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi na kuendeleza uhusiano.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili Dk Victor Ngota amesema upasuaji wa kuwatenganisha watoto unahitaji utaalamu wa hali ya juu hivyo ulihusisha jopo la wataalamu mbalimbali ikiwemo madaktari bingwa ikiwemo wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, wataalamu wa usingizi ,wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wa radiolojia.