HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa mara ya kwanza imezindua kliniki ya kupima kiwango cha mafuta katika mwili wa binadamu, ikiwa nchi ya nne kwa Afrika kuwa na aina hiyo ya kliniki.
Kliniki hiyo maalum itasaidia wagonjwa mbalimbali kama moyo na kisukari kujua kiasi cha mafuta, ili kuweza kukidhibiti kuepuka madhara zaidi.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo, Mkurugenzi wa MHN, Prof. Mohammed Janabi, alisema kliniki hiyo itaendeshwa kwa kushirikiana na Chuo cha Imperial kilichopo nchini Uingereza.
“Kilichofanyika leo kwa mara ya kwanza nchi yetu kupitia hospitali ya Taifa Muhimbili tumezindua hii kliniki ya mafuta, sisi ni nchi ya nne Afrika na zitakuwa zinafuatiliwa kimataifa na wenzetu wa nchi nyingine ni Somalia, Ethiopia na Sudan,” amesema.
Prof Janabi amesema faida ya kliniki hiyo ni kuwepo kwa wiki mara tatu kwa watu wazima na watoto, kwani mafuta yanasababisha magonjwa mengi moyo na kisukari.
Amesema faida nyingine ni madaktari wawili kwenda kusoma Uingereza, ili kuongeza ujuzi ambapo madaktari wa moyo na watoto ndio watakaokwenda.
“Magonjwa ya mafuta yanaweza kuja kwa njia nyingi wakati mwingine yanakuja katika ngozi na bahati mbaya wanapelekwa kwa madaktari wa ngozi kumbe tatizo ni mafuta, kliniki muhimu kwetu,”amesisitiza.
Ameeleza kuwa vifo asilimia 31 vinahusishwa na magonjwa ya moyo duniani, hivyo wanafurahi kupata nafasi na nchi itajulikana kwa huo utafiti mkubwa duniani.
Amebainisha kuwa takwimu za Muhimbili zinaonesha magonjwa ya moyo yako katika magonjwa 10 yanayoongoza, hivyo watakuwa wanatibu na kubwa zaidi watakuwa wanaelimisha jamii.