Mume anataka watoto 10, mke amefikisha nusu amechoka kuzaa!
*Alipoamua kutumia uzazi wa mpango, kapata mke mwenza
JOSEPHINE Mlay (sio jina lake halisi), mkazi wa Kijiji cha Songambele kilichopo Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, anasema hajui maisha yake yanaenda vipi, kwani yupo njia panda.
“Kile naweza sema ni kuwa ndoa sio safari rahisi kwa maana utakumbana na changamoto nyingi kuliko mafanikio, ukiwa na wakwe ambao wao ndio wasemaji wa mwisho kwenye ndoa yenu,” anasema.
Akizungumzia historia yake, anasema amekuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya miaka mitano, lakini sio ndoa ambayo alitamani.
Josephine mwenye umri wa miaka 27, ana watoto watano na anasema aliacha kusikilizana na wakwe zake punde tu alipojifungua mtoto wake wa tano ambaye kwa sasa ana miezi kadhaa.
“Mume ni mkulima, yeye hana kitu ila baba yake ana mali nyingi, ana ng’ombe zaidi ya 200, mume wangu hana sauti, anachosema baba yake ndicho anachofuata, baba yake anasema ni lazima mume wangu awe na watoto wengi, na mume wangu anamsikiliza na kusema anataka watoto 10 kutoka kwangu.
“Nimeng’ang’ana miaka yote kutekeleza yale wanayotaka lakini nimeona naweza kupoteza maisha, afya yangu ni dhaifu, na nimekuwa nikiumwa sana ninapobeba ujauzito, navimba miguu hadi nashindwa kutembea, mimba ya mwisho kidogo nipoteze maisha, lakini ni kama hawajali wanataka tu niendelee kuzaa.
“Kituo cha afya walinishauri kuhusu uzazi wa mpango, nilipomshirikisha mume wangu alikasirika sana akaenda kuwambia wakwe zangu, ndipo walipomtafutia mke mwingine,” anasema.
Anasema watoto wake watano wote wamepishana miezi kwa kuwa amezaa mfululizo bila ya kupumzika.
“Nimezaa mfululizo yaani nikijifungua ndani ya mwezi, hata sijakaa sawa najikuta na mimba nyingine, nimezaa mfululizo, nimechoka sana.
“Sikupata elimu ya afya ya uzazi wa mpango, nikibeba mimba naumwa sana, hadi nashindwa hata kufanya kazi, miguu inavimba nashindwa kutembea, mume wangu wala hajali anasema najidekeza.
“Anajiangalia yeye tu, napitia maumivu makali ukimwambia anasema unajidekeza mbona wengine wanaujauzito na wanaenda shambani kulima, na wanafanya kazi za nyumbani, anakua na hasira sana na mimi.
“Kila nikibeba ujauzito ni ugomvi tu na mume wangu mpaka najifungua, hajali kuwa na watoto wadogo, hajali changamoto ya afya ambayo napitia, yeye anachotaka ni kutimiziwa haja zake za mwili na ananiambia kabisa anataka tuzae watoto 10.
“Hali ile ilinichosha sana, kwa sasa nimepata elimu ya afya ya uzazi, nikamshirikisha kufunga uzazi alikasirika sana, akawashirikisha wazazi wake ambao nao walikasirika na kuamua kumuozesha mtoto wao mke mwingine.
“Mimi nimeshachoka sana na mambo ya kuzaa maana uhai wangu unakuwa hatarini kama mimba yangu ya mwisho nimeponea chupu chupu niliumwa sana na ujauzito ulitishia kutoka.
“Wamemuozesha mke mwingine ili aendelee kuzaa, unajua kabila lao baadhi ya watu wanaamini watoto wengi kama nguvu kazi, baba mkwe wangu ana ng’ombe 200 kwa sababu ya mali zake akasema lazima mwanae aoe mke mwingine; ….
“Wakamuozesha, binafsi nimeridhia kabisa acha na huyo mwenzangu naye azae tu hata akitaka kuongeza na mwingine ili amzalie aoe tu tuwe hata watatu wanne acha tu aoe, nimechoka sana,” anasisitiza.
UHABA WA VIPANDIKIZI HOFU YA MIMBA NYINGINE
Josephine, anasema kutokuwa na uhakika wa kupatiwa huduma ya njia ya uzazi ya vijiti kwa jina lingine vipandikizi inampa hofu ya kubeba mimba nyingine ya mtoto wa sita angali bado ana watoto wadogo waliofuatana huku wa mwisho akiwa bado ana nyonya.
“Ni zaidi ya mwezi sasa hakuna vipandikizi, hata wiki iliyopita nilikuja hapa kuangalia kama vimeshakuja lakini havipo, niliambiwa nikiona gari basi nije ndio itakua imeleta vifaa vya huduma ya uzazi wa mpango, lakini nimefika hapa pia naambiwa hakuna, sasa itanilazimu kuendelea kusubiri hadi itakapoletwa zahanati,” anasema.
Anasema amefika katika Zahanati ya Kamsisi kupatiwa huduma hiyo baada ya kupata taarifa kwamba gari lenye bidhaa hiyo lipo njiani linakwenda katika zahanati hiyo.
“Nimeona gari linakuja ndio nimeamua kulifuata. Lakini kumbe sio lililoleta vifaa, hapa ahanati waratibu walituambia tukiona gari ndio tuje, nimetoka kjiji cha mbali lakini mpango wangu wa kuweka njia ya uzazi wa mpango imekwama, nimekwazika sana,” anasema.
Akizungumza na HabariLEO, mtoa huduma katika kituo hicho cha Kamsisi, Adela Mwanda anakiri kuwa vitendea kazi ni hafifu na kwamba wakina mama hawana changamoto iwapo watapatiwa elimu ya uzazi wa mpango.
“Hapa kwetu vitendea kazi ni hafifu, lakini pia hakuna mtoa huduma ambaye alipatiwa mafunzo ya kupachika njia aina ya kitanzi, endapo tutapatiwa mafunzo itaturahisishia kutoa huduma ya kitanzi,” anasema na kuongeza:
“Tunapaswa tupatiwe mafunzo; kwa mfano mteja anakuja anataka huduma ya kitanzi, tunamjibu hakuna ila tunamshauri atumie njia nyingine.
“Kukosekana kwa huduma ya kitanzi hakutoi changamoto kwa mama kwa sababu tunamshauri aende kituo cha afya Inyonga B, ambacho kina wataalamu wa kutosha,” anasema Adela.
Kwa upande wa Ofisa Tabibu Msaidizi wa zahanati hiyo, Charles Wanguba anasema awali kituo cha Kamsisi kilikuwa kikipokea wateja 12, lakini kadiri siku zinavyosonga idadi ya wateja imeongezeka na kufikia 300 kwa mwezi.
“Nina miaka minne, nimeanza kazi zahanati ikiwa mpya; ilikuwa haipokei wagonjwa wengi, lakini taratibu idadi inazidi kuongezeka.
“Tulianza huduma ya akina mama kujifungua Desemba mwaka jana. Baadhi ya miundombinu ilikuwa imekaa vizuri, akina mama walikuwa wanakuja kidogokidogo ila kwa sasa idadi imeongezeka,” amesema na kuongeza kuwa kwa mwezi akina mama wanaojifungua ni asilimia 70 hadi 80.
Kwa mujibu wa Wanguba ni kwamba miongoni mwa changamoto zinazoikabili zahanati hiyo ni pamoja na upungufu wa watoa huduma na dawa.
Anasema walitegemea wawe na watoa huduma 15 lakioni waliopo sasa ni wawili tu.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mkoa wa Katavi wa Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto, Elida Machungwa, anasema kuwa baadhi ya njia hazipo katika baadhi ya vituo vya afya kutokana na kutokufanya makadirio vizuri ya uagizaji wa dawa kutoka kwa mamlaka za dawa nchini.
Kwa mujibu wa Machungwa ni kwamba Mkoa huo unapoingia katika changamoto ya aina hiyo ofisi inalazimika kuomba msaada kwa mikoa ya jirani wenye mzigo wa kutosha.
Pamoja na changamoto ya upungufu wa baadhi ya njia, upungufu wa watoa huduma waliopatiwa mafunzo pia umetajwa kuwa chanzo kinachochangia watumiaji wa njia ya uzazi wa mpango kukosa baadhi ya huduma ikiwemo vipandikizi.
Anasema changamoto inayoikabili Mkoa wa Katavi ni uchache wa watoa huduma na na baadhi ya vitendea kazi.
“Tunapenda tutoe huduma bora, changamoto yetu ni watoa huduma wachache, hakuna anayependa watu wakae kwenye foleni kwa muda mrefu,” anasema
MATUMIZI YA UZAZI WA MPANGO YAPUNGUA
Machungwa anasema kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni wastani wa asilimia 52 kwa wanawake walio kwenye ndoa mkoani Katavi na ambao hawako kwenye ndoa ni asilimia 22.
“Bado tunaendelea kuhamasisha watu watumie njia mbalimbali za uzazi wa mpango,” anabainisha.
TAKWIMU ZA UZAZI WA MPANGO TANZANIA
Kwa mujibu wa takwimu za Tanzania zilizowasilisha kwenye bunge la bajeti la mwaka wa fedha 2023/2024 zinaonesha katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 Serikali ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango 2,538,247 sawa na asilimia 89 ya lengo.
Sindano za uzazi wa mpango aina ya Depo-provera dozi 2,564,691 sawa na asilimia 94 ya lengo na vipandikizi 552,494 sawa na asilimia 81 ya lengo.
Aidha, katika kipindi cha taarifa hiyo jumla ya wateja 4,509,605 walitumia njia mbalimbali za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganishwa na wateja 4,905,854 kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.
Taarifa za Uedeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) zinaonyesha kuwa njia za uzazi wa mpango ambazo zilitumika katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 ni pamoja na vipandikizi (asilimia 45.7); Sindano (asilimia 22.8); vidonge (asilimia 12.6); kondomu (asilimia 11.6), vitanzi (asilimia 5.9); kufunga kizazi (asilimia 0.6); na njia nyingine (asilimia 0.9).
Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya wateja wapya 3,491,989 sawa na asilimia 60.7 ya wanawake walio wa umri wa kupata ujauzito waliotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganishwa na wateja 3,049,011 sawa na asilimia 62.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22.