MKAZI wa Manispaa ya Tabora anadaiwa kumuua mkewe na kumzika kwenye shimo katika chumba wanacholala na kusakafia eneo hilo kwa zege kutokana na kinachohisiwa ni wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Richard Abwao alisema ofisini kwake mjini Tabora jana kuwa tukio hilo la mauaji liligundulika Machi 7 mwaka huu saa 9.30 alasiri katika Mtaa wa Mbilani Kata ya Kidongo Chekundu.
Kamanda Abwao aliwaeleza waandishi wa habari kuwa mwananchi Michael Hendry ndiye aliyebaini hilo baada ya kuona siku kadhaa zimepita bila chumba hicho kufunguliwa. Alisema wananchi walivunja mlango wa chumba cha kulala na kukuta chini ya kitanda kuna zege iliyokuwa bado haijakauka vizuri.
Kamanda Abwao alisema walipata hofu hivyo wakafukua eneo hilo na kukuta mwili wa mtu umezikwa kwenye shimo hilo.
Alimtaja marehemu aliyekuwa amezikwa katika shimo hilo chumbani kwake (kwa marehemu) ni Salima Hamisi Maulid (34).
Kamanda Abwao alisema kwamba mtuhumiwa (jina limehifadhiwa) baada ya kutekeleza unyama huo alikimbia na jitihada za polisi zinaendelea kumtafuta.