Mume matatani kumchoma moto mkewe

MUME wa binti mwenye umri wa miaka 17 na watu wengine sita, wilayani Yumbe, wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi Yumbe kwa tuhuma za kumchoma moto mkewe wakimtuhumu kuiba.

Kaimu Msemaji wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Magharibi wa Nile, Ignatius Dragudu, alisema Sharon Driwaru (17), alichomwa moto na kundi la watu katika Kijiji cha Cwinya katika Halmashauri ya Mji wa Yumbe, Januari 8, mwaka huu kwa kutumia petroli.

“Polisi na baadhi ya wasamaria wema walimkimbiza binti huyo aliyeungua kiasi cha kutotambulika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Yumbe kwa matibabu.”

Advertisement

“Kwa mujibu wa uchunguzi, mwathirika huyo anadaiwa kuiba fedha za mama mzazi wa mume wake jambo ambalo mwenyewe alikanusha, lakini kundi hilo la watu likaamua kummwagia petroli na kumchoma moto,” alisema Dragudu.

Alisema: “Katika upelelezi tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba na mmoja wao alitambulika kuwa mume wa mwathiriwa. Watuhumiwa hao wamefunguliwa shitaka la kujaribu kuua na muda wowote watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka hayo.”

Taarifa ambazo hazijathibitishwa kutoka kwa jamii ya eneo hilo pia zinasema, Januari, 10, msichana mwingine chini ya umri wa miaka 14 aliuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana katika hoteli ya mtaa katika Soko la Edeku karibu na Makao Makuu ya Wilaya ya Yumbe.

Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya ya Yumbe, Mahad Azabo, alisema muda usiozidi mwezi mmoja, takribani watu 15 wameuawa wilayani humo na watuhumiwa wa uhalifu ambao ni vijana.

Mwenyekiti wa Wilaya ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Abdulmutwalib Asiku, alisema kamati yake imechukua hatua kadhaa kupambana na uhalifu wilayani hapa.