Mume mbaroni akidaiwa kumchinja mkewe

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limemkamata Mapinduzi Siliya (45) akituhumiwa kumuua mkewe, Terezia Mtajiha kwa kumchinja kwa kutumia kisu na kisha kuutupa mwili katika mto Nzovwe.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema jana tukio hilo ni la Januari 11 mwaka huu saa 7 mchana katika Kata ya Nzovwe Tarafa ya Iyunga mkoani humo baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mkewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.

Majirani wa wanandoa hao walidai kuwa mtuhumiwa huyo na mkewe wamekuwa na ugomvi wa mara kwa mara na walipokuwa wakijaribu kuwasuluhisha, Siliya alikuwa akiwatishia kuwapiga.

“Hawa watu maisha yao ilikuwa ni kipigo kila siku wakitoka kunywa pombe huko utasikia kelele tu, tukienda kuamulia anaenda kuchukua rungu kubwa tunaogopa. Juzi mimi tuligombana akanitishia akasema wewe usicheze na damu yangu, sasa jana tu walipita na mke wake wako vizuri tu, leo balozi ananipigia simu mchana kuwa Mapinduzi kamchinja mke wake,” alisema Willy Simpasya.

Jirani mwingine, Aziza Kiula alidai kuwa Siliya na mkewe walikuwa wakiongozana kila mahali lakini wakati wa usiku walikuwa wakigombana mara kwa mara.

Habari Zifananazo

Back to top button