Museveni ashutumu mataifa ya Magharibi kushadadia ushoga

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amezishutumu nchi za Magharibi kwa kuweka haki za wapenzi wa jinsi moja kwa mataifa ya Afrika huku wabunge nchini humo wakijiandaa kupigia kura muswada dhidi ya LGBT.

Muswada huo uliowasilishwa mapema mwezi huu, unapendekeza adhabu kali zaidi kwa mahusiano ya jinsi moja katika nchi ambayo ushoga tayari ni kinyume cha sheria.

Imezua ukosoaji kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Katika hotuba yake bungeni juzi, Rais Museveni alisema vitisho vya Magharibi vya kuwekea vikwazo nchi za Kiafrika zinazopinga ushoga ni vya kinafiki kwa sababu nchi za Magharibi pia zina tamaduni za ajabu.

“Nchi za Magharibi zinafaa kukoma kupoteza wakati wa ubinadamu kwa kujaribu kulazimisha mazoea yao kwa watu wengine,” alisema Rais Museveni.

“Wazungu na makundi mengine huoa binamu na jamaa wa karibu, hapa kuoa mtu katika ukoo ni mwiko. Je, tuwawekee vikwazo kwa kuoa jamaa? Hii si kazi yetu,” aliongeza.

Chini ya sheria iliyopendekezwa, mtu yeyote anayejihusisha na mapenzi ya jinsi moja au anayejitambulisha kuwa LGBT anaweza kufungwa jela miaka 10.

Serikali za Magharibi na mashirika ya misaada yanayofanya kazi nchini Uganda yanashutumiwa mara kwa mara kwa kukuza ushoga nchini humo.

Habari Zifananazo

Back to top button