Museveni mambo shwari
UGANDA: RAIS Yoweri Museveni anatarajiwa kufanyiwa kipimo cha mwisho cha Covid-19 kesho ili kubaini kama amepona ugonjwa huo.
Museveni, ambaye amekuwa akijitenga tangu Juni 7 baada ya kuambukizwa Covid-19, anatarajiwa kurejea kazini mara moja iwapo vipimo vitabainika kuwa hana maambukizi.
Hayo yalibainishwa wakati wa maombi ya kitaifa yaliyofanyika katika ofisi ya mwenyekiti wa taifa iliyopo Kyambogo, Kampala, jana. Maombi hayo yaliandaliwa ili kumwomba Mungu amponye Rais Museveni.
Ndugu yake, Shadrack Nzeire Kaguta aliwaomba waumini kumtakia Bw Museveni ahueni ya haraka.
“Rais tayari hayuko hatarini, niliwasiliana naye jumatatu kwa njia ya simu na akaniambia yuko sawa na kwa kufuata taratibu za kawaida za uendeshaji kutoka Wizara ya Afya anasubiri kipimo cha mwisho pengine Alhamisi, wiki hii,” alisema.
“Rais… ameanza majukumu yake ya kawaida kama vile kushughulikia baadhi ya majalada akiwa peke yake,” Bw Nzeire aliongeza.
Aidha alisema wanaowatakia wengine kifo ni walaji nyama kwa sababu huwezi kushangilia wakati mtu mwingine anaumwa.
“Sote tuna damu moja, bila kujali itikadi za kisiasa…sote tumeumbwa na Mungu tuache chuki zote hizi tupendane maana akifa wewe unafuata,” alisema.