Museveni: Wabunge EU wana mawazo finyu

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amesema Mradi wa Ujenzi wa Bomba Ghafi la Mafuta Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima nchini humo hadi Chongoleani mkoani Tanga utaendelea kama ulivyopangwa.

Museveni amewaponda wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) kwa kuupinga mradi huo, akisema walichokisema Septemba 16, mwaka huu ni mawazo finyu kwa kudhani wanajua kila kitu.

Wabunge hao walipitisha azimio la kutaka mradi wa EACOP usimame kwa mwaka mmoja wakidai kuna ukiukwaji wa haki za binadamu.

Akifungua Mkutano wa Kimataifa wa Mafuta na Gesi jijini Kampala juzi, Rais Museveni alilitaka Bunge la EU litulie kwa kuwa si uwanja sahihi wa vita kwao.

“Jambo muhimu ni kwamba tunaendelea na programu yetu. Bunge la Ulaya lina mambo mengi ya kufanya kwao. Nawashauri watumie muda zaidi kumaliza matatizo ya watu pale. Afrika Mashariki ina watu wenye uwezo wanaoelewa nini cha kufanya,” alisema Rais Museveni.

Alihimiza kampuni za mafuta ziendelee na kazi ya ujenzi wa bomba na mitambo ya kusafisha mafuta na anatumaini wadau wataliunga mkono hilo.

Alisema awali hakuunga mkono wazo la kujenga bomba hilo na akataja sababu mbili za kubadili msimamo huo ikiwamo ya kuwezesha Watanzania kunufaishwa na mradi huo kwa kuwa walisaidia harakati za kujikomboa.

Alitaja sababu ya pili kwamba Tanzania na Msumbiji zina gesi nyingi ukilinganisha na Uganda hivyo mradi huo utawezesha kujengwa bomba la nishati hiyo kuipeleka nchini kwake.

Septemba 23, mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilieleza Bunge kuwa mradi huo utatekelezwa kwa kuzingatia sheria za Tanzania na za kimataifa.

Alisema mradi huo utatekelezwa kwa uwazi, tahadhari za kimazingira, ulinzi wa mifumo ya kiikolojia na rasilimali za maji, masuala ya kijamii, kijinsia na haki za binadamu kwa ujumla na kuwataka wadau wote wasiwe na hofu.

Alisema mradi wa EACOP una manufaa kwa Tanzania na Uganda na umefanyiwa tathmini ya kimazingira kuhakikisha utekelezaji wake hauna athari za kimazingira kwa jamii.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Adrian Mbilinyi
Adrian Mbilinyi
2 months ago

Hongera sana Mheshiwa Raisi Mseveni ipo haja ya watanzania na waganda kuungana na viongozi wetu wakuu kuwashanga EU kwa kuacha mambo yao makuu ulaya na kuingilia ‘mradi wa inchi maskini kama UGANGA NA TANZNIA” EU acheni Roho mbaya

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x