Musk amrejesha Trump Twitter

MMILIKI wa Twitter na Bosi wa Tesla, Elon Musk amerejesha akaunti ya Twitter ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.
Akaunti hiyo, ambayo ilifungiwa kufuatia shambulio la Januari 6, 2021, kwenye Capitol, imerejeshwa baada ya Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Twitter na mmiliki mpya kuhoji watumiaji wa Twitter ikiwa Trump anafaa kurejeshwa.
“Watu wamezungumza. Trump atarejeshwa,” Musk ameandika kwenye Twitter mapema leo. “Vox Populi, Vox Dei,” akaongeza kwa kilatini akimaanisha “Sauti ya watu ni sauti ya Mungu.”
The people have spoken.
Trump will be reinstated.
Vox Populi, Vox Dei. https://t.co/jmkhFuyfkv
— Elon Musk (@elonmusk) November 20, 2022
Hadi Jumapili asubuhi, saa za Tanzania, asilimia 51.8 ya kura milioni 15 zilizopigwa kwa siku mbili zilitaka Trump arejeshwe. Asilimia 48.2 ya kura hizo hawakutaka Trump arejee katika jukwaa hilo.
Uamuzi huo unaweka mazingira ya kurejea kwa rais huyo wa zamani kwenye mtandao wa kijamii ambapo hapo awali alikuwa na ushawishi mkubwa zaidi, ikiwa ni mtumiaji mwenye utata. Akiwa na karibu wafuasi milioni 90, tweets zake mara nyingi ziliweka mzunguko wa habari na kuendesha ajenda huko Washington.
Akaunti inayoonekana kwa sasa ni ya @realDonaldTrump ikiwa na wafuasi milioni1.
Trump alisema hapo awali angesalia kwenye jukwaa lake, Truth Social, badala ya kujiunga tena na Twitter, lakini mabadiliko katika mtazamo wake yanaweza kuwa na athari kubwa za kisiasa. Rais huyo wa zamani alitangaza mwezi huu kwamba atawania uteuzi wa urais wa Republican mwaka wa 2024, akilenga kuwa kamanda mkuu wa pili kuwahi kuchaguliwa kwa mihula miwili tofauti.