Muswada bima ya afya kwa wote waahirishwa
MUSWADA wa Bima ya Afya kwa Wote uliokuwa ujadiliwe bungeni na kukamilika hatua zote tatu kabla ya kuwa sheria, umeahirishwa hadi hapo mashauriano kati ya Bunge na serikali yatakapokamilika.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, muswada huo haukusomwa kwa mara ya pili na tatu jana kutokana na kuwapo mambo ambayo hawajaafikiana na serikali hivyo umeondolewa katika ratiba ya shughuli za jana ambako Bunge liliahirishwa.
Katika orodha ya shughuli za Bunge, kulikuwa na hati za kuwasilishwa mezani na kwamba hati hizo zilitakiwa kuwasilishwa na Waziri wa Afya na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. “Sasa hati hii haitawasilishwa leo mezani kwa sababu Bunge pamoja na Serikali tunaendelea na mashauriano juu ya mambo ambayo hatujaafikiana vizuri,” alisema Spika Dk Tulia.
Aliongeza: “Bunge hilo halitautazama muswada huo tena ambao kwa mara ya kwanza ulisomwa katika mkutano uliopita na kupelekwa kwa kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.” Alisema ratiba ni kuwa muswada huo ulikuwa uingie jana bungeni kwa mjadala na kumaliza kazi ya kuitunga sheria.
Dk Tulia alisema wanaendelea na mashauriano katika hoja kadhaa zilizoibuliwa na wabunge, wadau mbalimbali waliojitokeza katika kamati na nyingine serikali inaendelea kuzitazama namna bora ya kuwahudumia kwenye eneo hili la bima ya afya kwa wote.
Alisema muswada huo utapelekwa bungeni watakapokuwa wameshakamilisha mashauriano hayo. Muswada huo uliwasilishwa bungeni katika Mkutano wa Nane wa Bunge uliofanyika Septemba mwaka huu baada ya kuahirishwa kwa miaka kadhaa.